` ACHANA NA WATEJA TASA – ONGEZA FAIDA YA BIASHARA YAKO

WANDAMAN HOTEL

ACHANA NA WATEJA TASA – ONGEZA FAIDA YA BIASHARA YAKO


 

ACHANA NA WATEJA TASA – ONGEZA FAIDA YA BIASHARA YAKO

                                                                  na Shinyanga Press Club.

Wafanyabiashara wengi hukwama kwa sababu wanategemea wateja wale wale kila mwaka na kila msimu. Wakati huo huo, gharama za biashara kama kodi, mishahara, vifaa, usimamizi na teknolojia zinaendelea kuongezeka. Hali hii ni hatari kwa ukuaji wa biashara na inaweza kuifanya idhoofike au hata kufa.

Mfanyabiashara anaweza kuwa na wateja 80 kwa muda mrefu bila kuongeza idadi yao. Hata kama wateja hao ni waaminifu, biashara haiwezi kukua kwa kasi ikiwa haipanui soko lake. Ukuaji wa biashara unategemea uwezo wa kuongeza wateja wapya kila wakati.

Kuongeza wateja kunaleta manufaa mengi, ikiwemo kuongeza mauzo, kupanua mtandao wa biashara, kujenga thamani ya chapa (brand), kupata fursa mpya za kibiashara na kuongeza mapato.

Ili kuongeza wateja kutoka 80 hadi 200 au zaidi, mfanyabiashara anapaswa kuwekeza katika teknolojia, kujifunza mbinu mpya za biashara, kusoma mabadiliko ya soko na kutoridhika na mafanikio ya sasa. Biashara inayokua ni ile inayotafuta wateja wapya kila siku.

Kadiri biashara yako inavyojulikana na kuaminika, ndivyo idadi ya wateja na mauzo inavyoongezeka. Lengo si kubaki na kundi lile lile la wateja, bali kupanua wigo wa soko kila wakati.

Kwa mfano, ikiwa biashara yako inafikiwa na watu 2,000 na asilimia 10 tu watanunua, utapata wateja 200. Lakini ukiifikia hadhira ya watu 200,000, hata kama asilimia 10 pekee watanunua, utakuwa na wateja 20,000. Hapo ndipo nguvu ya kuongeza wigo wa soko inapodhihirika.

Njia za kuongeza wateja ni pamoja na:Kufungua matawi mapya,kutafuta masoko mapya,kutumia teknolojia na mitandao ya kijamii kutangaza biashara,kushirikiana na wadau wengine ndani ya sekta yako,kuboresha njia za usambazaji wa bidhaa au huduma na kutoa huduma bora zinazowafanya wateja kukupendekeza kwa wengine.

Biashara nyingi zinazoshindwa kuongeza wateja hubaki "tasa", hukosa ukuaji, hupungua taratibu na hatimaye hufungwa.

Usikubali biashara yako ibaki na wateja wale wale mwaka hadi mwaka. Ongeza wigo wa soko, ongeza wateja, na utaongeza faida.

Endelea kufuatilia Shinyanga Press Club kwa maarifa ya biashara, ujasiriamali na maendeleo kila siku.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464