` WANANCHI ZAIDI YA 40,000 SHINYANGA WAFAIDIKA NA MSAADA WA KISHERIA

WANDAMAN HOTEL

WANANCHI ZAIDI YA 40,000 SHINYANGA WAFAIDIKA NA MSAADA WA KISHERIA

 

Wanasheria na wataalamu wa ardhi wakiendelea kuelimisha na kutoa elimu ua msaada wa kisheria katika kata ya Iselamagazi wilaya ya Shinyanga vijijini 

Na Suzy Butondo, Shinyanga

Zaidi ya wananchi 40,000 katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamenufaika na kampeni ya msaada wa kisheria inayotekelezwa na serikali, huku wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wakipatiwa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia na haki zao za msingi.

Mbali na elimu hiyo, wananchi pia wamepewa uelewa kuhusu makosa ya jinai, migogoro ya ardhi pamoja na masuala ya ukatili wa kijinsia, ambayo yamekuwa changamoto kubwa katika jamii.

Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Shinyanga, wakiwemo wakazi wa Kata ya Iselamagazi, wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni hiyo ya msaada wa kisheria ambayo imewasaidia kupata ushauri wa kisheria na kutatuliwa baadhi ya migogoro iliyodumu kwa muda mrefu.

Wananchi hao walitoa shukrani hizo leo baada ya kupatiwa elimu na ushauri wa kisheria katika kituo cha Iselamagazi, wilayani Shinyanga.

Mkazi wa Kata ya Iselamagazi, Ndila Ndege, alisema alikuwa na mgogoro wa ardhi kwa zaidi ya miaka mitano bila kupata suluhu, lakini kupitia kampeni hiyo ameweza kuelewa hatua za kisheria zinazopaswa kufuatwa.

“Nimepata huduma na ushauri mzuri. Naiomba serikali ya Mama Samia iendelee kutusaidia ili tuweze kuishi kwa amani katika maeneo yetu,” alisema Ndege.

Naye Maganga Masanja Katina wa Kijiji cha Mwabundala alisema alipatiwa ushauri wa kufungua shauri la mirathi baada ya familia yao kushindwa kugawana urithi wa hekta 53 zilizoachwa na baba yao kwa zaidi ya miaka miwili.

“Tulikuwa hatuelewi kuwa tayari mahakama ilishatoa maamuzi ya kugawana urithi. Tumeelekezwa kwenda kufungua shauri la mirathi ili kila mmoja apate haki yake,” alisema Masanja.

Mwanasheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Anthony Sakani, alisema wananchi wengi bado hawana elimu ya kutosha kuhusu sheria jambo linalochangia kuendelea kwa migogoro katika jamii.

Alisema changamoto kubwa zilizojitokeza katika kampeni hiyo ni migogoro ya ardhi na mirathi, huku wananchi wengi wakipatiwa elimu na ushauri uliowasaidia kuelewa namna ya kutatua migogoro yao kwa njia za kisheria.

“Tangu zoezi lianze tumewafikia wananchi wengi vijijini na mashuleni katika wilaya hii ya Shinyanga ni zaidi ya wananchi 40,000 wamenufaika na msaada wa kisheria, ambapo tumetoa elimu kuhusu haki za watoto na ukatili wa kijinsia,” alisema Sakani.

Kwa upande wake, Afisa Mipango Miji wa Wilaya ya Shinyanga, Petro Alphonce, alisema mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa tangu kuanza kwa kampeni hiyo tarehe 6,5,2026

Alisema zoezi hilo limewezesha wananchi wengi kupata elimu, ushauri pamoja na utatuzi wa migogoro mbalimbali, huku akiwahimiza wale ambao bado hawajapata huduma kujitokeza kupata msaada wa kisheria, ambao mwisho wa kampeni hiyo katika wilaya ya Shinyanga itakuwa 20,5,2026


Wanasheria na wataalamu wa ardhi wakiendelea kuelimisha na kutoa elimu ua msaada wa kisheria katika kata ya Iselamagazi wilaya ya Shinyanga vijijini 

Wanasheria na wataalamu wa ardhi wakiendelea kuelimisha na kutoa elimu ua msaada wa kisheria katika kata ya Iselamagazi wilaya ya Shinyanga vijijini 
Afisa Mipango Miji wa Wilaya ya Shinyanga, Petro Alphonce,akizungumza baada ya kutoa huduma











Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464