

Salum Maige, Geita.
Wachimbaji wadogo katika mgodi wa Msasa Halmashauri ya Bukombe mkoani Geita wameipongeza serikali kuanza hatua za kuwapelekea nishati ya umeme ikiwa ni hatua za kuwanusuru na matumizi ya mafuta kuendesha mitambo yao.
Mgodi huo unaokadiriwa kuwa na zaidi ya wachimbaji 10,000 umeanza tangu disemnba mwaka jana na kukusanya maelfu ya wananchi wakiwemo wafanyabiashara.
Kufuatia uwepo wa shughuli hizo tayari serikali imeanza kupeleka nishati ya umeme katika eneo hilo kwa kuweka nguzo ili kuhakikisha tangwa la wachimbaji hao kuwarahisia shughuli za uchimbaji linatimia.
Kwa mujibu wa meneja wa Mgodi huo Kessy Maira amesema, wanaipongeza serikali kwa kusikia kilio chao na kuanza hatua za kuwafikisha nishati ya umeme wa Tanesco ili kuwaepusha na matumizi ya mafuta.
“Tunatumia gharama nyingi za mafuta, lakini umeme ukianza kutumika , tutaepukana na kutumia mafuta na kazi zitafanyika kila wakati, kwani kuna muda mafuta yakiisha inabidi msimame kwanza uzalishaji” amesema Maira.
Meneja wa shirika la Umeme Tanzania mkoa wa Geita Jahulula Maendeleo amesema upatikanaji wa umeme katika mkoa huo ni megawati 70.5 na kwamba mkakati wa sasa katika mkoa ni kuhakikisha vitongoji 528 vilivyosalia vinafikiwa na umeme.
Baadhi ya maeneo aliyoyataja ni pamoja kufikisha umeme kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo likiwemo eneo la Msasa.
“Msasa tayari umeme umeshafika inachofanyika ni kufikisha nguzo kwenye maduara ili sasa kuhakikisha adhima ya serikali ya kufikisha umeme kwenye machimbo inatimia” anasema Maendeleo.
Aidha, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amesema hadi kufikia Mei 2026, jumla ya migodi 289 ya wachimbaji wadogo imepatiwa umeme ikiwemo migodi 18 katika Jimbo la Lupa wilayani Chunya mkoani Mbeya ambayo ni pamoja na migodi ya Singa, Chokaa Moja, Mapogoro, Godima Beston, Matfra, Mwambe Mlimanjiwa, Mamboleo, Mbiwe na Mwaoga mbili.
Mhe. Salome ameyasema hayo Mei 15, 2026 katika Kikao cha 30 cha Mkutano wa tatu wa Bunge la 13 unaoendelea bungeni jijini Dodoma alipokua akijibu swali la Mbunge wa Lupa, Mhe. Masache Kasaka aliyehoji mpango wa serikali wa kupeleka umeme kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo.
Aidha Mhe. Salome amesema Serikali kupitia kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme katika maeneo ya wachimbaji wadogo wa madini, mashamba ya kilimo na viwanda katika mikoa yote nchini ambapo mpango uliopo kwa sasa ni kufikisha umeme katika maeneo 308 ya wachimbaji wadogo ifikapo Juni 2027.
“Serikali kupitia REA itaendelea kupeleka umeme katika migodi midogo midogo iliyosalia ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kuunganisha umeme katika migodi yao”. Amesema Mhe. Salome.
Mwisho.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464