
Wagombea wa nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 wamemmwagia sifa na pongezi nyingi Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia uamuzi wake wa kuunda Tume ya Uchunguzi wa Kijinai wa Matukio ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu.
Hatua hiyo ya rais imekuja ikiwa ni utekelezaji wa haraka wa mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 iliyokuwa chini ya Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman.
Viongozi hao wamempongeza Rais Samia kwa kuonyesha nia thabiti ya kuliponya taifa kwa kutumia Sheria ya Tume za Uchunguzi kuunda chombo hicho maalum kitakachoshughulikia viashiria vyote vya jinai vilivyobainika.
Miongoni mwa waliotoa pongezi hizo ni aliyekuwa mgombea urais kupitia chama cha Makini, Coster Kibonde, aliyempongeza rais kwa weledi mkubwa alioonyesha katika kuteua majaji wastaafu na wabobezi wa sheria nchini, akiamini kuwa uteuzi huo unaenda kumaliza 'kiporo' cha kipelelezi kilichoachwa na ripoti ya kwanza.
Pongezi hizo ziliungwa mkono na aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Kunje Ngombale Mwiru, aliyesifu uamuzi huo akieleza kuwa kuundwa kwa tume hiyo ni jambo jema linalolenga kuweka uwiano mzuri wa mwenendo wa usalama wa taifa.
Viongozi hao wamebainisha kuwa uamuzi wa rais kuweka hadharani ukweli utasaidia kwa kiasi kikubwa kutibu majeraha ya Oktoba 29 na kuimarisha msingi wa maridhiano ya kitaifa.