` MATUMAINI MAKUBWA YATAWALA KUWA TUME YA MAJAJI WASTAAFU ITATENDA HAKI BILA UPENDELEO

WANDAMAN HOTEL

MATUMAINI MAKUBWA YATAWALA KUWA TUME YA MAJAJI WASTAAFU ITATENDA HAKI BILA UPENDELEO


Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu
Wadau wa siasa na waliokuwa wagombea urais nchini wameonyesha kuwa na matumaini makubwa kuwa Tume ya Uchunguzi wa Kijinai iliyoundwa hivi karibuni itatenda haki kikamilifu na kuondoa kabisa hofu na malalamiko ya wananchi kuhusu uwajibikaji.

Tume hiyo, inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Shabani Ally Lila akisaidiana na makamishna ambao ni majaji wastaafu Gad Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir, na Aishieli Sumari, inatarajiwa kufanya upelelezi wa kina ili kubaini wahusika wa ghasia, vifo, na majeraha.

Wadauhao hao wameeleza kuwa wana imani kubwa na wajumbe hao kutokana na rekodi zao za uadilifu, wakiamini kuwa watafanya kazi kwa mujibu wa sheria ili kuleta majibu yataridhisha na kuweka wazi ukweli utakaotibu majeraha ya kijamii.

Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA), Salum Mwalimu, ameeleza matumaini yake kuwa kuwepo kwa tume hiyo kutasaidia kuanza kwa uwajibikaji wa kweli, hatua itakayofanya mioyo ya watu ipoe na kurejesha utayari wa wananchi kushirikiana kama taifa moja.

Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha UMD, Mwajuma Mirambo, aliongeza kuwa wana matumaini makubwa kwa sababu chombo hicho kimeundwa na watu sahihi watakaosikiliza maoni ya wanajamii na kuleta mwarobaini wa jinsi ya kujenga taifa lenye umoja na amani.

Ili tume hiyo iweze kutenda haki na kufanya kazi yake kwa ufanisi, viongozi hao wametoa wito kwa Watanzania kuwa watulivu na kuepuka kuendesha midahalo inayoweza kuingilia au kuvuruga mwenendo mzima wa uchunguzi huo wa kijinai.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464