` VIJANA LINDENI AMANI YA TANZANIA

WANDAMAN HOTEL

VIJANA LINDENI AMANI YA TANZANIA

                                      

Na. Vero Ignatus

Mwanadiplomasia na Mratibu wa Makongamano ya Vijana, Ndugu Omary Abdul Punzi, ametoa onyo kwa vijana nchini kuacha kufuata mikumbo isiyo na tija na badala yake waithamini nchi yao kwa kutanguliza uzalendo mbele. 

Akizungumza katika mahojiano maalum na Vuka Blog, Punzi amesisitiza kuwa amani ya nchi haitofautiani na utulivu wa kisiasa, bali inategemea kwa kiasi kikubwa jinsi vijana wanavyoheshimu utamaduni wao na kushirikiana kikamilifu na mihimili nane muhimu inayolinda na kulea taifa. 

Amewasihi vijana kuwa makini na ushawishi hasi wa utandawazi na makundi yasiyo na maadili yanayotishia mustakabali wa nchi.

Akionyesha masikitiko yake, Punzi amekumbusha kuwa Tanzania ni urithi wa thamani tulioachiwa na waasisi wetu, hivyo hakuna nchi nyingine mbadala ikiwa vijana wataharibu hii iliyopo. 

Alibainisha kuwa miongozo na desturi nzuri zilizowekwa na wazee wa kimila tangu zamani hazikuwa za kizamani, bali zililenga kulinda utu na heshima ya jamii. 

Alionya kuwa sasa vijana wanatupa dhahabu yao kwa sababu tu inaonekana ya kienyeji na kuokota shaba ya kigeni kwa kuwa inang’aa, jambo linalohitaji mabadiliko ili mila na desturi zilizokubalika zisafishwe na kuendelezwa badala ya kufutwa kabisa.

Katika uchambuzi wake, Punzi alifafanua jinsi mihimili nane ya amani na malezi inavyopaswa kuwa dira kwa kijana mzalendo. Mhimili wa kwanza ni shule ambayo ndiyo msingi wa maarifa, nidhamu na malezi ya awali ya kiakili yanayomfanya kijana kuwa raia mwema. 

Hii inaenda sambamba na Jeshi la Polisi ambalo ni chombo cha usalama wa raia na mali zao kinachotegemea ushirikiano wa karibu na vijana kupitia ulinzi shirikishi. 

Vivyo hivyo, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linatajwa kama jukwaa la kuwajenga vijana katika ukakamavu na uzalendo, huku Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) likiwa ngome kuu ya ulinzi wa mipaka ya nchi na alama ya mamlaka ya taifa.

Mihimili mingine inayokamilisha ngome hii ya malezi na ulinzi inajumuisha Idara ya Usalama wa Taifa, chama cha Skauti, taasisi za kidini, pamoja na mila na desturi nzuri ambazo ndizo msingi wa utambulisho wa Mwafrika unaosisitiza heshima, mshikamano na utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo badala ya vurugu. 

Punzi amewataka vijana kutokubali kuwa bendera inayofuata upepo wa mambo yanayoonekana maarufu kwenye mitandao ya kigeni, kwani kufanya hivyo ni kupoteza dira.

 Alizitaka taasisi zote za elimu, dini na vikosi vya usalama kushirikiana kwa karibu ili kuwatengenezea vijana mazingira wezeshi yatakayowafanya kuwa walinzi namba moja wa amani na maendeleo ya Tanzania.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464