` NAIBU WAZIRI AYOUB AWATAHADHARISHA VIJANA USAMBAZAJI TAARIFA POTOFU

WANDAMAN HOTEL

NAIBU WAZIRI AYOUB AWATAHADHARISHA VIJANA USAMBAZAJI TAARIFA POTOFU


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud, ametoa onyo kali kwa vijana nchini akisisitiza kuwa hawapaswi kabisa kutumia teknolojia kueneza chuki, uchochezi na taarifa potofu zinazoweza kuvuruga mshikamano wa wananchi na kuhatarisha usalama wa taifa. 

Amesema kwa sasa kuna wimbi kubwa la taarifa potofu zinazosambaa kwa kasi, hivyo ni wajibu wa kila kijana kuwa makini, kufanya utafiti kabla ya kuamini au kusambaza jambo, na kuwa mstari wa mbele kulinda amani na usalama wa taifa kwa kuepuka vitendo vyote vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.

Akizungumza katika Jukwaa la Maendeleo ya Vijana Tanzania linalofanyika jijini Dodoma na kukutanisha jumla ya vijana 600 kutoka mikoa mbalimbali nchini, Naibu Waziri Ayoub amebainisha kuwa dunia ya sasa inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiusalama zikiwemo migogoro ya kijamii na mivutano ya kisiasa.

Ameongeza kuwa matumizi mabaya ya teknolojia na mitandao ya kijamii ndiyo yanayochochea kwa kiasi kikubwa changamoto hizo, hali inayotaka umakini wa hali ya juu kutoka kwa nguvukazi hiyo ya taifa ili kuzuia mifarakano katika jamii.

Kiongozi huyo amekumbusha kuwa amani ndiyo msingi mkuu na wa pekee wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa nchini, na bila hiyo hakuna jambo linaloweza kufanikiwa. Kutokana na ukweli huo, amewasihi vijana kote nchini kujenga utamaduni wa kuwa wazalendo wa kweli na kutunza tunu hiyo muhimu ya amani kwa manufaa makubwa ya vizazi vya sasa pamoja na vizazi vijavyo.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464