A

Tishio la Viongozi ‘Wapopulisti’: Jinsi Ushawishi wa Kisaikolojia Unavyolikausha Taifa na Jukumu la Vijana Kulilinda
Na Beda Msimbe, BSKY Media

Katika ulimwengu wa sasa wa kisiasa, kuna mstari mwembamba sana kati ya harakati za kutetea wananchi na siasa za hila zinazolenga kujenga umaarufu binafsi. 
Siasa hizi za "upopulisti" (populism), ambapo viongozi huahidi wananchi "mbingu na nchi" huku wakitumia mbinu za kisaikolojia kuwateka wafuasi wao, zimetajwa kuwa tishio kubwa linalomeng'enya misingi ya utaifa, huku zikiacha makovu ya kiuchumi na kijamii ambayo athari zake hudumu hata baada ya serikali husika kuondoka madarakani.

Onyo hilo limetolewa na Mwanasiasa mkongwe na Mbunge wa zamani wa Nyamagana, Ezekia Wenje, wakati akizungumza Mei 16, 2026, kwenye Kongamano la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu lililoandaliwa na TAHLISO katika ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam. 

Kongamano hilo lililobeba kaulimbiu ya ‘Never Again: Tuipende, Tuitunze, Tuilinde Nchi Yetu’, lililenga kuwakumbusha vijana wajibu wao mkuu wa kulinda nchi bila kuongozwa na ushabiki wa kiitikadi.

Mtego wa Kisaikolojia: Kutoka kwa Wanasiasa hadi "Kondoo"

Akichambua kitabu maarufu cha How to Lose a Country: The Rise of Populist Leaders and Activists, Wenje alieleza kuwa viongozi wapopulisti wana mbinu hatari ya kutengeneza mifumo ya kifikra (cults) inayofanya wafuasi wao wakubali na kufuata kila wanachoambiwa bila kuhoji.

 Mtego huu wa kisaikolojia haunasi watu wasio na shule pekee, bali unawateka hata wasomi ambao hujikuta wakishabikia maamuzi yanayobomoa nchi zao wenyewe.

Wenje alitolea mfano wa jinsi Uingereza ilivyojiondoa kwenye Umoja wa Ulaya (Brexit) baada ya wanasiasa wapopulisti kuwaaminisha wananchi kuwa wanapoteza fedha nyingi, lakini matokeo yake sasa yamekuwa mzigo mkubwa wa kiuchumi.

 Alikwenda mbali zaidi na kukumbusha tukio la kihistoria la kutisha la Jim Jones nchini Marekani, aliyewateka wafuasi wake kisaikolojia, akawahamishia nchini Guyana, na hatimaye kuwanyonyesha sumu watu zaidi ya 900 kwa ahadi za kwenda mbinguni.
"Hata huko nyuma nilikotoka mimi (CHADEMA), tulikuwa tumetengeneza 'cult' (mfumo wa kuabudu viongozi). Ukimwambia mtu aandamane, anaandamana tu hata kama hajui sababu ya kuandamana wala matokeo yake," alikiri kwa uwazi Wenje, akisisitiza umuhimu wa kutumia msemo wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete: "Akili za kuambiwa, changanya na za kwako."
Gharama ya Vurugu: Somo la Oktoba 29 na Jinamizi la Ukimbizi

Akirejea matukio yaliyotikisa nchi mnamo Oktoba 29, 2025, Wenje alibainisha kuwa athari za kisiasa zikitafsiriwa kuwa vurugu, zinaleta umasikini wa kudumu. Alitolea mfano wa mama mmoja aliyekutana naye mkoani Mwanza akiomba msaada baada ya kupoteza ajira kufuatia kuchomwa moto kwa kiwanda cha magodoro cha mkoani humo siku hiyo ya vurugu.

Akinukuu ripoti ya Jaji Chande, Wenje alisema hasara ya vurugu hizo ilifikia Shilingi bilioni 100, huku bilioni 89 zikiwa zimepotea kutoka sekta binafsi. 

Alieleza kuwa uharibifu wa miundombinu kama vituo vya mafuta unavuruga mnyororo mzima wa kiuchumi (ecochain)—kuanzia walinzi, wauza mafuta, waendesha bodaboda, hadi wamachinga na mama ntilie wanaotegemea mzunguko huo.

"Ukishachoma moto nchi yako, unabaki na nini? Serikali zinapita lakini nchi inabaki. Ukiondoka kwenda nchi yoyote kukaa nje kwa sababu ya kuivuruga nchi yako, wewe utakuwa mkimbizi tu," alionya Wenje, akitolea mfano wa uchaguzi wa mwaka 2007 nchini Kenya uliosababisha zaidi ya watu 6,000 kuwa wakimbizi wa ndani (IDPs).

Maridhiano Ndiyo Nguzo; Hakuna Upande Unaojipatia 100%

Mwanasiasa huyo alishambulia vikali tabia ya baadhi ya viongozi wa sasa wanaokataa vikao vya maridhiano, akisema kiongozi yeyote anayekataa meza ya mazungumzo hana mapenzi ya dhati na Taifa. Alieleza kuwa migogoro mikubwa duniani, ukiwemo ule wa ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini chini ya Nelson Mandela na F.W. de Klerk, na hata migogoro ya sasa ya Mashariki ya Kati, hatimaye humalizwa kwa njia ya mazungumzo.

Alikumbusha jinsi alivyokuwa "kijana" wa mwanasiasa wa Kenya, Raila Odinga, mwaka 2007 wakati Kofi Annan alipoenda kusuluhisha nchi hiyo, na jinsi Odinga alivyomshauri Freeman Mbowe kutochagua njia ya kususa uchaguzi kwani ingekiua chama cha CHADEMA. Mbowe alielewa na kuchukua njia ya diplomasia—tofauti na viongozi wa sasa wanaoendekeza misimamo mikali (hardline).

"Katika maridhiano, hakuna upande unaopata asilimia 100; ni suala la kutoa na kupokea (give and take). Hata tulipokuwa Bunge la Kumi tukaanzisha UKAWA, tulichukua msimamo mkali na kususia Bunge la Katiba kwa sababu ya kudai serikali tatu. 
Leo hii najuta, tulitakiwa kubaki kwani katiba ile ilikuwa na mambo mengi mazuri sana. Katiba sio msahafu, tungeikubali na yale mapungufu tungeendelea kuyarekebisha mbele ya safari," alieleza Wenje kwa masikitiko.

Wito kwa Vijana: Kataeni Kupangiwa Maandamano Kutoka Nje
Wenje alitoa rai kwa vijana nchini kuto kubali kutumiwa kama chambo na watu waliopo salama nje ya nchi—iwe Nairobi au Marekani—ambao hutumia majina ya bandia (pseudo names) kwenye mitandao ya kijamii kuwahamasisha vijana kuingia barabarani kufanya fujo.

"Mtu yupo salama huko nje, anakuambia nenda kaandamane, ameshakupampu kisaikolojia, nawe kama kondoo unaenda. Lazima vijana mtambue nchi ni kubwa kuliko mtu yeyote. Kazi yenu kubwa ni kuilinda nchi yenu, msikubali kupotezwa na viongozi wapopulisti," alihitimisha Wenje.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464