` TAKUKURU YATIKISA SHINYANGA,FEDHA ZA MRADI ZAREJESHWA BAADA YA UFUATILIAJI

WANDAMAN HOTEL

TAKUKURU YATIKISA SHINYANGA,FEDHA ZA MRADI ZAREJESHWA BAADA YA UFUATILIAJI



Na Suzy Butondo, Shinyanga

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kurejesha zaidi ya shilingi milioni 21 kupitia ufuatiliaji wa matumizi ya fedha, uchunguzi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na utoaji wa elimu kwa umma.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi 2026, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, amesema fedha hizo zimeokolewa kupitia ufuatiliaji wa mradi wa ujenzi wa Shule Mpya ya awali na Msingi Tinde B iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Kessy amesema pia kuwa TAKUKURU iliendesha semina kwa viongozi wa Vyama vya Msingi vya Kilimo na Masoko (AMCOS) Wilaya ya Kishapu, hatua iliyosaidia kuongeza uelewa kuhusu namna ya kufuatilia madai yao dhidi ya baadhi ya makampuni ya ununuzi wa zao la pamba.

Ameeleza kuwa katika juhudi za kuzuia rushwa, taasisi hiyo ilifanya ufuatiliaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan mradi wa ujenzi wa shule hiyo, na kubaini kuwa fedha hazikuwa zimelipwa kama ilivyostahili.

“Kupitia mapendekezo yaliyotolewa na ufuatiliaji uliofanywa, fedha zote zililipwa katika mamlaka husika,” amesema Kessy.

Aidha Kessy ametoa wito kwa taasisi zote za umma kutoa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia misingi ya maadili, pia wananchi wote wa mkoa wa Shinyanga amewaomba kushirikiana kikamilifu na TAKUKURU katika juhudi za kuzuia na kupambana na rushwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma za kijamii kwa ujenzi wa jamii.

"Wananchi wote niwaombe mkipata taarifa yeyote inayoashiria rushwa mtoe taarifa kupitia namba 113 bure kwani kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu, hivyo niwaombe tutimize wajibu wetu"amesema Kessy

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464