.jpg)
Suzy Butondo, Shinyangapressblog
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kukamata silaha moja aina ya bastola TISAS yenye namba za usajili T0620-22J00122 pamoja na risasi 11 zilizokuwa ndani ya magazine yake.
Silaha hiyo iliripotiwa kuibwa katika tukio la wizi lililotokea Mei 10, 2026 katika mtaa wa Nyakato, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amesema bastola hiyo ilikuwa ikimilikiwa kihalali na Richard Mhabi (38), mfanyabiashara na mkazi wa Nyakato, Kahama.
Kamanda Magomi amesema kuwa baada ya uchunguzi na operesheni maalumu zilizofanywa na jeshi hilo, watuhumiwa wawili wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo na wanaendelea kushikiliwa kwa ajili ya hatua za kisheria.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limefanikiwa pia kuwakamata wahamiaji haramu 11 waliokuwa wameingia na kuishi nchini bila vibali katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Aidha, polisi wamekamata vielelezo mbalimbali ikiwemo lita za mafuta ya dizeli, mabati 558, kete 228 za bangi, lita 115 za pombe haramu aina ya moshi, kilogramu 89 za mirungi, pikipiki 11 pamoja na betri tatu za magari.