
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa imepokea vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya shilingi milioni 120 kutoka Shirika la Chakula Duniani (WFP), kwa lengo la kuimarisha vituo vya operesheni na mawasiliano ya dharura pamoja na utekelezaji wa mfumo wa Anticipatory Action (AA).
Vifaa hivyo vinavyojumuisha kompyuta za mezani, runinga kubwa tatu za inchi 100 pamoja na mashine za kuchapisha, vimekabidhiwa Mei 12, 2026 katika hafla iliyofanyika katika ofisi za WFP jijini Dodoma na kuzinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Senyamule amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi na majanga mbalimbali, huku akisisitiza umuhimu wa taarifa kuwafikia wananchi kwa wakati na kwa ufanisi.
“Vifaa hivi vitaongeza ubora na ufanisi wa taarifa zinazowafikia wananchi kwa haraka ili waweze kuchukua tahadhari dhidi ya maafa yanayoweza kutokea,” amesema Mhe. Senyamule huku akiishukuru WFP kwa mchango wake katika kuimarisha sekta ya menejimenti ya maafa nchini.
Kwa upande wake, Naibu Mwakilishi Mkazi wa WFP, Bi. Christine Mendes amesema tafiti zinaonyesha kuwa uwekezaji katika maandalizi na kinga dhidi ya majanga ni nafuu zaidi kuliko gharama za kukabiliana na madhara baada ya majanga kutokea. Amesema ushirikiano huo unalenga kujenga ustahimilivu na maendeleo endelevu ya jamii.
Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni na Uratibu wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (SBUU), Kanali Selestine Masalamando amesema vifaa hivyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha mfumo wa Taifa wa menejimenti ya maafa na kuongeza uwezo wa kukabiliana na majanga yanayoikumba nchi.
Kanali Masalamando ameongeza kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuimarisha ufuatiliaji wa vihatarishi, utoaji wa tahadhari za mapema, ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za maafa pamoja na kuboresha uratibu na mawasiliano kati ya ngazi ya Taifa, mikoa na wilaya wakati wa majanga.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464









