` JAJI AWATAKA WATANZANIA KUWA NA TABIA YA KUTOA SHUKURANI KUWEZESHA AMANI

WANDAMAN HOTEL

JAJI AWATAKA WATANZANIA KUWA NA TABIA YA KUTOA SHUKURANI KUWEZESHA AMANI


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, ametoa wito mzito kwa Watanzania, hususan vijana, kujenga utamaduni wa kutoa shukrani kama nguzo muhimu ya kuimarisha amani ya ndani na kuepusha machafuko katika jamii.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kitabu cha mashairi kiitwacho Sing Gratitude kilichoandikwa na Wakili Msomi Aisha Saidi Kingu, Jaji Masaju alibainisha kuwa shukrani ni kielelezo cha unyenyekevu ambacho kinapungua kwa kasi katika ulimwengu wa sasa unaotawaliwa na ubinafsi.

Alisisitiza kuwa hali ya kisiasa na kijamii nchini inategemea sana uwezo wa watu kutambua michango ya wenzao, kwani pale unyenyekevu unapokosekana, ugomvi na kutovumiliana huchukua nafasi na kuhatarisha mshikamano wa kitaifa.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Mei 10, 2026 kwenye ukumbi wa Mlimani City na kuhudhuriwa na viongozi wa kijeshi, mabalozi, na majaji, Mhe. Masaju alifafanua kuwa shukrani ina faida lukuki kisaikolojia ikiwamo kupunguza msongo wa mawazo na hisia za hasira au wivu.

Alieleza kuwa jamii yenye shukrani hujenga uhusiano wa heshima na mshikamano, kwani watu wanapohisi kuthaminiwa, hujitolea zaidi kushirikiana katika ujenzi wa taifa.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, muujiza mkubwa wa mabadiliko ya kijamii unapatikana katika neno "asante," ambalo linavuta uwepo wa Mungu na kuleta utukufu unaounganisha binadamu pasipo kujali tofauti zao.

Akihusisha dhana hiyo na maandiko matakatifu, Jaji Mkuu alirejea kitabu cha Isaya 9:6 na Wathesalonike, akisisitiza kuwa shukrani ni amri ya kiungu inayoleta amani na kuepusha shari.

Alionya kuwa kizazi cha sasa kinakabiliwa na hatari ya kupoteza baraka na uelekeo kwa sababu ya kuacha asili ya kushukuru, hali inayopelekea watu kuona kila wanachofanyiwa ni haki yao badala ya fadhila. Jaji Masaju alitoa rai kwa Watanzania kurudi katika misingi ya mila na desturi za kushukuru ili kumaliza changamoto na migogoro kwa njia ya mazungumzo, jambo ambalo ni msingi wa maadili ya kitanzania.

Mhe. Masaju pia aliwataka Watanzania kuunga mkono waandishi wa ndani na kutambua michango ya wazazi na walimu, akisisitiza kuwa taifa linalowapa vijana nafasi ya kubuni na kuandika linajenga urithi imara wa maarifa na mshikamano kwa vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, mwandishi wa kitabu hicho, Wakili Aisha Saidi Kingu, alieleza kuwa lengo la kazi yake ni kuwakumbusha watu umuhimu wa kutambua baraka ndogo na kubwa katika maisha ili kusonga mbele kwa matumaini.

Wakili Aisha alibainisha kuwa kuchagua kushukuru kwenye udogo ndiko kunakomfungulia mtu milango ya ukubwa, huku akionyesha ndoto yake ya kuona vijana wa Kitanzania wakikua katika maadili mema na kutumia vipaji vyao kuelimisha jamii.

Viongozi wa dini walioshiriki uzinduzi huo, Sheikh Issa Othman Issa na Padri Faustine Furaha, waliunga mkono hoja hiyo kwa kunukuu vitabu vitakatifu vya Quran na Biblia, wakisisitiza kuwa shukrani ni tunda la uvumilivu. Walieleza kuwa moyo usiokuwa na shukrani hukausha mema yote na kwamba kuhesabu baraka huleta zingine nyingi.

Kitabu hicho, ambacho kimeandikwa kwa mfumo wa mashairi, kimeelezwa na wachambuzi Bw. Joram Nkumbi na Dkt. Ishmail Mwambapa kuwa ni kazi bora ya kifasihi inayoweza kushindana kimataifa na kupata tuzo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464