` HAKUNA MAENDELEO KAMA HAKUNA AMANI-NANAUKA

WANDAMAN HOTEL

HAKUNA MAENDELEO KAMA HAKUNA AMANI-NANAUKA

Amani ndiyo msingi wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na bila utulivu hakuna maendeleo yatakayodumu hapa nchini.

 Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, ambaye alisisitiza kuwa serikali inatamani kuona nguvu za vijana zikitumika kwenye ubunifu, kazi, na uchumi badala ya kupotezewa kwenye siasa za chuki. 

Waziri Nanauka alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la wanafunzi wa vyuo vikuu lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) lililojadili nafasi ya vijana katika kulinda amani, mshikamano, na maendeleo ya taifa, ambapo viongozi mbalimbali walitoa onyo kali kwa vijana dhidi ya kujiingiza kwenye siasa za chuki, propaganda za mitandaoni, na migawanyiko ya kijamii.

Katika kongamano hilo, viongozi wa serikali, wasomi, na wanasiasa walipaza sauti zao kwa pamoja wakikumbusha kuwa vijana wanapaswa kuwa walinzi wakuu wa mshikamano wa kitaifa badala ya kukubali kutumiwa kama chambo cha kisiasa. 

Waziri Nanauka alihimiza kwa nguvu zote umuhimu wa kuepuka ubaguzi wa dini, ukabila, na itikadi kali za kisiasa ambazo zinaweza kuhatarisha umoja na usalama ambao taifa limeujenga kwa miaka mingi.

Alibainisha kuwa serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kupitia sera mbalimbali, mikopo, na mifumo ya zabuni za umma ili kuwainua vijana kiuchumi, na kuongeza kuwa wizara yake itaendelea kusaidia miradi ya vijana katika sekta za maji, Tehama, na shughuli nyingine za kiuchumi ndani ya Wilaya ya Ubungo na nchini kote.

Akiitolea ufafanuzi Sera ya Maendeleo ya Vijana, Waziri Nanauka alieleza kuwa imekuwa chachu ya kutungwa kwa sheria inayozilazimu halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya makundi maalum ya vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu. 

Vivyo hivyo, Sheria ya Manunuzi ya Umma inaelekeza asilimia 30 ya zabuni za halmashauri kuelekezwa kwa makundi hayo, ambapo asilimia 10 ya kiwango hicho ni maalum kwa vijana pekee. 

Katika mwaka wa fedha uliopita, fursa zenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni tatu zilikuwa wazi kwa ajili ya vijana kupitia mfumo wa manunuzi ya umma, ingawa waziri alibainisha masikitiko yake kuwa ushiriki wa vijana katika Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) bado upo chini sana, huku kukiwa na vikundi visivyozidi 3,000 nchi nzima. 

Ili kurekebisha hali hiyo, serikali imeweka mkakati wa kusajili zaidi ya vikundi 20,000 ndani ya miaka mitano ili viweze kunufaika na zabuni hizo na kujikwamua kiuchumi.

Kuhusu malalamiko yanayotolewa mara kwa mara juu ya ugumu wa kupata mikopo, Waziri Nanauka alifafanua kuwa vikwazo vingi vinaepukika iwapo wahusika watafuata taratibu na kuwa na nia ya dhati. 

Alitolea mfano wa kijana mmoja aliyekuwa akilalamika mtandaoni kwenye mtandao wa Instagram kuhusu masharti magumu, ambapo baada ya waziri kufuatilia kwa siri na kumpigia simu, alibaini kuwa kijana huyo aliona sharti la kuwa na kitambulisho au barua ya utambulisho kuwa ni ngumu mno. 

Waziri alimweleza kijana huyo kuwa hakuna mahali popote duniani ambapo mtu anaweza kupewa mkopo bila utambulisho wa kisheria, huku akisisitiza kuwa changamoto nyingi zinazovumishwa mitandaoni zinaweza kutatulika kwa urahisi kama vijana wakizingatia misingi na taratibu zilizowekwa. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464