WAHITIMU VETA WAOMBA MITAJI KUPAMBANA NA UKOSEFU WA AJIRA
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
WAHITIMU 107 wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mkoani Shinyanga, wameiomba serikali kuwapatia mitaji kupitia mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri ambayo asilimia nne hutolewa kwa wanawake na vijana na asilimia mbili watu wenye ulemavu, ili waweze kujiajiri baada ya kuhitimu mafunzo yao.
VIDEO👇👇
Ombi hilo limetolewa leo Mei 15, 2026 wakati wahitimu hao wakisoma risala kwenye mahafali ya 46 ya daraja la tatu ya chuo hicho, kwa mgeni rasmi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa Fadhili Maganya.
Akisoma risala hiyo kwa niaba ya wahitimu wenzake Daniel Kolowa, amesema licha ya changamoto mbalimbali walizokumbana nazo chuoni hapo, sasa wanakwenda kukabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira baada ya kuhitimu.
Amesema kutokana na wao kuwa na ujuzi wa kazi mbalimbali, wanaomba serikali iwasaidie kupata mitaji kupitia mikopo ya vijana ya halmashauri, ili waweze kujiajiri na kukabiliana na tatizo hilo la ajira.
Mkuu wa Chuo cha Veta Shinyanga Abrahamu Mbughuni, amesema mbali na mafaniko ya Chuo hicho bado kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo uchakavu na uchache wa mitambo, upungufu wa vyumba vya madarasa, kuharibika kwa uzio wa chuo na kuhatarisha usalama wa wanafunzi na mali za chuo hicho.
Naye Mgeni Rasmi Fadhili Maganya, amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, kwamba atengeneze vikundi kuanzia vitatu hadi vine vya wahitimu hao na kuvisimamia, ili vipate mikopo ya Halmashauri ya asilimia 10, na kuwa kama mfano wa kuigwa katika kujiajiri na kuweza kunufaika na mikopo hiyo.
Aidha, amesema baadhi ya changamoto ambazo zimewasilishwa watakwenda kuzifanyia kazi.
TAZAMA PICHA👇👇
Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa fadhili Maganya akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Mkurugenzi wa fedha VETA Fidelis Tungu akizunguma kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA Taifa.
Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga Abraham Mbughuni akizungumza.
Mhitimu Daniel Kolowa akisoma Risala.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464