
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Shinyanga, Sheikh Balilusa Khamis, ameiomba serikali kutozipuuza kauli zinazotolewa na baadhi ya watu, hususan viongozi wa kijamii na kisiasa, ambazo zinaweza kuhatarisha usalama wa wananchi na utulivu wa taifa wachukuwe hatua kali.
Akizungumza katika mahojiano maalum katika muktadha wa kuimarisha mshikamano wa kijamii, amesema kuna mwenendo unaojitokeza wa baadhi ya watu kutoa maneno yasiyo na staha na yasiyo sahihi, jambo ambalo linaweza kuchochea taharuki na migogoro isiyo ya lazima endapo halitachukuliwa hatua mapema na kuhatarisha amani na utulivu.
Aonya Madhara ya Kauli za Uchochezi
Mwenyekiti wa kamati ya amani amesisitiza kuwa suala la amani si la kubezwa, bali ni jukumu la msingi la serikali kulinda na kuhakikisha linaendelea kudumu wakati wote. Ameonya kuwa mtu mmoja mwenye kauli potofu anaweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii, akieleza kuwa historia imeonesha kuwa migogoro mingi huanzia kwenye maneno yasiyopimwa.
“Ni muhimu watu wakakemewa mapema, Kauli zisizo na msingi zinaweza kuleta maafa makubwa, Serikali inapaswa kuwa makini na kuchukua hatua dhidi ya upotoshaji unaoendelea,” amesisitiza Balilusa
Amesema Tume ya kuchunguza matukio ya wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 imefanya kazi kubwa na inahitaji kuungwa mkono kwa kuyafanyia kazi mapendekezo yake ili kuchukuwa hatua.
Vijana Wakumbushwa Kutambua Historia ya Taifa
Katika nasaha zake kwa vijana, amewataka kutambua mabadiliko chanya yaliyopatikana nchini kwa kulinganisha maisha ya sasa na ya zamani, Amesema vijana wanaolalamikia hali ya maisha wanapaswa kuwauliza wazee wao ili kuelewa safari ya maendeleo iliyopatikana ikilinganishwa na zamani.
Ameeleza kuwa tofauti na zamani ambapo huduma muhimu kama umeme na miundombinu bora zilikuwa adimu, kwa sasa kumekuwa na maboresho makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, makazi na huduma za kijamii.
Aidha, amekosoa tabia ya baadhi ya watu kulinganisha maisha ya Tanzania na nchi nyingine bila kuzingatia mazingira halisi ya kila taifa, amesema mtazamo huo unaweza kupotosha fikra za wananchi na kuondoa ari ya kujivunia na kujenga nchi yao.
“Tunapaswa kujivunia tulichonacho na kuendelea kukijenga. Kukimbilia kulinganisha na mataifa mengine ni hatari kwa ustawi wa taifa letu,” amesema.
Amebainisha kuwa katika baadhi ya nchi, migogoro imekuwa ikichochewa na kauli za wanasiasa wanaopotosha ukweli ili kujijengea umaarufu, Hali hiyo, amesema, inaweza kujitokeza pia endapo jamii haitakuwa makini na kuchambua taarifa wanazozipokea.
Kwa upande mwingine, amewasihi vijana kujenga utamaduni wa kuchuja na kuthibitisha taarifa kabla ya kuzichukua kama ukweli. Amesema kukubali kila kinachosemwa bila uchunguzi kunaweza kusababisha maamuzi yasiyo sahihi na hatimaye kuhatarisha amani ya nchi.
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa jukumu la kulinda amani ni la kila Mtanzania, akiwataka wananchi wote kushirikiana na serikali katika kukemea vitendo na kauli zinazoweza kuvuruga utulivu uliopo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464