Suzy Butondo, ShinyangaBlog

Mkuu wa Chuo cha Calvary Reform Bible Institute Tanzania, Lawrence Daffa, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya pili ya Philadelphia Bible College, amewataka wahitimu kudumu katika mzizi wa imani, kuishi katika uhalisia wa nyakati na kuwa na ustahimilivu wanapofanya kazi ya Mungu.

Akizungumza katika mahafali hayo yaliyofanyika katika eneo la Ndembezi mjini Shinyanga, Daffa amesema wahitimu hao wa ngazi ya cheti wanapaswa kumtumikia Mungu kwa uhalisia, ustahimilivu na kudumu katika mizizi ya imani.

“Nyinyi ndiyo wabeba ushuhuda huo, hivyo leo ningependa niwaagize mambo matatu, mdumu katika mzizi wa imani, msiruhusu elimu yenu ya kitaaluma kuchukua nafasi ya ukaribu wenu na Roho Mtakatifu,  kadiri mnavyoendelea kupanda juu, ndivyo Roho Mtakatifu anavyopaswa kuwa karibu zaidi nanyi,” amesema Daffa.

Aidha amesema wahitimu wanapaswa kuishi kwa kutambua uhalisia wa nyakati wanazoishi.

“Pili, niwaombe mdumu katika uhalisia wa nyakati. Eleweni majira mnayoishi kama wana wa Isakari. Biblia inasema katika 1 Nyakati 12:32 kuwa wana wa Isakari walitambua nyakati. Hivyo na nyinyi mna uwezo wa kusikia sauti ya Mungu na kuelewa mnachotakiwa kufanya,” amesema.

Daffa pia amewataka wahitimu kuwa na ustahimilivu katika utumishi wao.

“Biblia inasema siku za mwisho zitaleta mashinikizo, lakini kumbukeni kwamba Roho aliyemfufua Kristo kutoka kwa wafu anaishi ndani yenu,” amesema.

Amesema vyeti walivyopata ni alama ya kujitoa kwa ubora, hivyo hawapaswi kuwa na huduma ya kawaida wakati wanamtumikia Mungu wa mambo makuu yasiyoonekana, pia amewataka ndugu wa wahitimu wasiopuuzie wito wa Mungu wanapopokea mguso wa kiroho.

“Biblia inasema mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache, tunaandaa watumishi kwa sababu siku za mwisho zinajulikana kuwa ni nyakati za hatari, hatuwahitaji watumishi wenye mwanga hafifu, tunahitaji wenye moto na nguvu, mtume Paulo alimwambia Timotheo katika 2 Timotheo 3:1 kwamba siku za mwisho zitakuwa za hatari, hivyo nendeni mkamtumikie Mungu kwa nguvu zote,” amesema Daffa.

Aidha, amewakaribisha watu kujiunga na chuo hicho kwa ajili ya kupata elimu ya kiroho.

“Karibuni katika Chuo cha Philadelphia mpate elimu ya kimungu. Mahali hapa ukisoma utakutana na nguvu ya Mungu. Tuna walimu wazuri, hivyo Mungu awaguse katika kumtumikia,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Philadelphia Bible College, Askofu Baraka Laizer, amesema wataendelea kusimamia mafunzo hayo ili kupata watumishi wenye neno la Mungu na moyo wa utumishi





















Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464