Na Marco Maduhu, SHINYANGA
WATU wawili Kisaka Elinihaki (22) na Makoye James (20), wamehukumiwa kifungo jela baada ya kupatikana na hatia ya kusambaza taarifa za uongo zilizozua taharuki kwa wananchi wilayani Kahama, mkoani Shinyanga kuwa wamepoteza nyeti zao.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga lilisema watuhumiwa hao walikamatwa Aprili 7, 2026, wakiwa wakazi wa Manispaa ya Kahama, wakitoa taarifa za uongo kuwa sehemu zao za siri zimepotea baada ya kuguswa bega, hali iliyosababisha hofu kubwa katika jamii.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Aprili 9, 2026 na kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi, kwamba baada ya watu hao kifikishwa Mahakama ya Wilaya ya Kahama, walipatikana na hatia ya kusambaza taarifa hizo za uongo kupoteza nyeti zilizosababisha taharuki.
Kamanda amesema, Katika hukumu hiyo Kisaka Elinihaki alihukumiwa kifungo cha miezi sita jela, huku Makoye James akihukumiwa kifungo cha miezi mitano jela.
Aidha, amesema Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga limeonya kuwa, kusambaza taarifa za uongo ni kosa la jinai, na kunaweza kusababisha taharuki pamoja na kuvuruga utulivu wa jamii.
Aidha, wamewataka wananchi kutoa taarifa sahihi na kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kudumisha amani na utulivu.
