` VIJANA WAHIMIZWA KUTUMIA UBUNIFU NA KAZI KULINDA AMANI NA MSHIKAMANO WA KITAIFA

WANDAMAN HOTEL

VIJANA WAHIMIZWA KUTUMIA UBUNIFU NA KAZI KULINDA AMANI NA MSHIKAMANO WA KITAIFA

Vijana nchini wamehimizwa kutumia nguvu na vipaji vyao katika shughuli za ubunifu na uzalishaji mali badala ya kujiingiza katika vitendo vya vurugu vinavyoweza kuhatarisha amani na mustakabali wa maisha yao. 

Baraka Masusani, mkazi wa Manispaa ya Shinyanga, ametoa mwito huo akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi mkuu wa maendeleo, na vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuilinda kwa kupinga chuki na migogoro. 

Katika kuunga mkono kampeni ya kitaifa ya maridhiano na utulivu, Masusani amebainisha kuwa ushawishi wa makundi yasiyofaa na kukaa vijiweni bila kazi maalum ni miongoni mwa vichocheo vinavyowafanya baadhi ya vijana kutumika vibaya, jambo ambalo linaweza kusababisha kupoteza maisha, uhuru, na heshima ndani ya jamii.

Ili kujikwamua kiuchumi na kuimarisha mshikamano, vijana wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta za kilimo, biashara ndogondogo na teknolojia ili kujenga maisha yenye tija na tishio lolote kwa usalama wa nchi. 

Masusani ameeleza kuwa badala ya kutumika katika harakati za uvunjifu wa amani, vijana wanapaswa kuwa chachu ya mabadiliko kupitia kazi halali zinazochangia pato la taifa na ustawi wa familia zao. 

Kwa upande wake, James Peter, mkazi wa Kata ya Ndembezi, ameongeza kuwa jamii ina wajibu mkubwa wa kushirikiana katika kuwapa vijana elimu sahihi ya maadili ili waweze kufanya maamuzi bora yanayolinda utulivu wa nchi yetu.

Msisitizo huo unakuja wakati huu ambapo taifa linaendelea kusisitiza umuhimu wa maridhiano na umoja, ukikumbusha kuwa kwa kushikamana na kufanya kazi kwa bidii, vijana wanaweza kuwa walinzi imara wa amani. 

Kwa kutambua thamani ya maisha yao na kuepuka vitendo vya kihalifu na matumizi ya dawa za kulevya, vijana wanajijengea mazingira salama ya kutimiza ndoto zao. 

Hivyo, mwito umetolewa kwa kila kijana kutathmini mchango wake katika taifa na kuhakikisha kuwa anakuwa sehemu ya suluhisho la kudumisha Tanzania kuwa kisiwa cha amani na utulivu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464