
Umoja na mshikamano miongoni mwa
wananchi ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo ya taifa, huku wito
ukitolewa kwa kila Mtanzania kuendelea kuilinda na kuitunza amani iliyopo ili
kudumisha mazingira bora ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumza katika mahojiano maalum,
mchimbaji mdogo wa madini Shinyanga David Elias amesema kuwa amani ndiyo
inayowawezesha wananchi kufanya shughuli zao kwa uhuru na utulivu, jambo
linalochochea uzalishaji na kukuza kipato .
Amesema ni jukumu la kila mwananchi
kuhakikisha analinda amani kwa nguvu
zote, akibainisha kuwa bila amani hakuna kazi yoyote inayoweza kufanyika kwa
ufanisi, hali ambayo inaweza kurudisha nyuma juhudi za maendeleo.
“Mazingira ya amani yanatupa fursa
ya kufanya kazi zetu kwa utulivu kabisa bila usumbufu wowote. Tunapata muda wa
kuzalisha na kuboresha maisha yetu na familia zetu,” amesema mchimbaji huyo.
Amesema kukosekana kwa amani
kunaweza kusababisha hali mbaya ikiwemo watu kuishi kwa hofu na hata kulazimika
kukimbia makazi yao, hali ambayo inaweza kuifanya jamii kugeuka kuwa kama
wakimbizi ndani ya nchi yao wenyewe.
Ameongeza kuwa mshikamano wa kijamii unapaswa kuendelezwa kwa kuvumiliana, kuheshimiana na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za maendeleo, hatua itakayosaidia kuimarisha umoja wa kitaifa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464