SERIKALI SHINYANGA KUUNDA JUKWAA KUDHIBITI WATOTO WANAOISHI NA KUFANYA KAZI MITAANI
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
SERIKALI wilayani Shinyang, imepanga kuunda jukwaa kwa ajili ya kudhibiti wimbi la watoto ambao wanaishi na kufanya kazi mitaani, ili warudi kuishi katika familia zao na kutimiziwa haki zao za msingi. kwa mujibu wa sheria ya mtoto ya 2009 ikiwamo elimu.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 23,2026 na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, kwenye kikao cha wadau wa masuala ya mtoto, yakiwamo mashirika, Wenyeviti wa mitaa, watendaji wa kata, maafisa maendeleo ya jamii, ustawi, viongozi wa dini, madiwani, na Jeshi la Jadi Sungusungu.
Mtatiro amesema, ili kudhibiti kabisa wimbi la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, katika Manispaa ya Shinyanga na wilaya ya Shinyanga, wanaunda Jukwaa maalumu ambalo litahusika na tatizo hilo, ili kusiwepo tena na watoto hao mitaani bali warudi kuishi majumbani mwao.
“kuanzia kesho tunaunda jukwaa la kudhibiti wimbi la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, jambo la pili lifanyike zoezi la kubaini watoto wote ambao wanaishi mitaani, na taarifa yake ninaitaka ifikapo Mei 5 mwaka huu,” amesema Mtatiro.
Aidha, amesema kupitia kamati yake ambayo aliiunda awali, kuwa watoto hao wengi wanatoka hapo hapo Shinyanga na ni wachache tu, ndiyo wanatoka nje na mkoa.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Thubutu Afrika Initaitives Jonathan Manyama, na Mwenyekiti wa Mashirika yanayopambana na ukatili wa kijinsia mkoani Shinyanga, amesema baada ya kuona ripoti za Nipashe kuhusu tatizo la watoto wa mitaani, walikuwa na mapendekezo yao kwa serikali, juu ya kuundwa kwa kamati itakayoshughulikia tatizo hilo, ambalo tayari serikali ilikuwa na mpango wa kuiunda.
Nao baadhi ya washiriki wa kikao hicho wakiwamo Wenyeviti wa serikali za mitaa, wamesema ili kumaliza tatizo hilo la watoto wa mitaani, pande zote zinapaswa kuwajibika wazazi pamoja na serikali.
katika kuibua tatizo hilo la wimbi la watoto wa mitaani Shinyanga, Gazeti la Nipashe mnamo Februari 2026 lilichapisha mfululizo wa ripoti maalumu tatu zilizoangazia maisha ya watoto wa mitaani, ambapo Februari 12 lilichapisha ripoti yenye kichwa “Watoto hadi hospitali wafunguka magumu yao usalama ukibaki rehani”, Februari 13 “Kasi ya ongezeko la watoto wa mitaani Shinyanga yashtua”, na Februari 16 “Wadau wadai uwajibikaji wa kweli kulinda haki za watoto.”
Ripoti hizo ndizo zimesababisha viongozi, viongozi wa serikali na mashirika, kuchukua hatua ya kidhibiti wimbi hilo la watoto wa mitaani Shinyanga, ili warudi kuishi majumbani mwao na kutimiziwa haki zao kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 kupitia vifungu vya 6(1)(d), 7 na 9, inaeleza mtoto ana haki ya kulelewa na wazazi au walezi wake, kupewa jina na utaifa, pamoja na kupata mahitaji ya msingi yakiwamo chakula, malazi, mavazi, matibabu, chanjo, elimu na haki ya kucheza na kuburudika.
Pia, Kanuni za usalama wa mtoto za mwaka 2014 (zilizofanyiwa marekebisho mwaka 2019) zinaeleza kuwa mtoto anatakiwa kuishi katika familia yake au sehemu salama pamoja na kulindwa dhidi ya aina yoyote ya vitendo vya ukatili.
MAELEZO YA PICHA NA VIDEO KWA CHINI👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza kwenye kikao hicho.
Mkurugenzi wa Shirika la Thubutu Afrika Initaitives Jonathan Manyama, na Mwenyekiti wa Mashirika yanayopambana na ukatili wa kijinsia mkoani Shinyanga, akizungumza.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464