Na Marco Maduhu, SHINYANGA
KLINIKI ya kuwahudumia wagonjwa wa Himofilia imezinduliwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, huku waganga wa tiba asili wakitahadharishwa kuacha kuhusisha ugonjwa huo na imani za kishirikina.
Uzinduzi huo umefanywa leo Aprili 21, 2026 na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Timoth Sosoma, ambaye amesema wagonjwa wa himofilia wanapaswa kupata matibabu sahihi hospitalini badala ya kupelekwa kwa waganga wa jadi.
Amesema, ugonjwa huo ni wa kurithi na husababisha damu kushindwa kuganda kwa urahisi, na kusababisha mgonjwa kuvuja damu mfululizo, hivyo haupaswi kuhusishwa na ushirikina.
“Leo tumezindua rasmi Kliniki ya wagonjwa wa himofilia katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, ugonjwa huu usihusishwe na imani za kishirikina, mwenye tatizo la kutokwa damu mfululizo afike hospitali kupata matibabu sahihi,” amesema Sosoma.
Ameeleza kuwa hadi sasa Mkoa wa Shinyanga una wagonjwa wanne waliobainika kuwa na himofilia, huku akiwataka wataalamu wa afya waliopatiwa mafunzo maalumu kuhakikisha wanatoa huduma kwa usahihi.
Sosoma pia amewasisitiza wafamasia kujaza taarifa sahihi za wagonjwa, ili kurahisisha upatikanaji wa dawa kutoka kwa wafadhili.
Katibu wa Chama cha Himofilia Tanzania Abdallah Makala na msimamizi wa mradi, amesema ugonjwa huo husababisha damu kushindwa kuganda mwilini, hivyo mgonjwa anapopata jeraha huvuja damu kwa muda mrefu na kuhatarisha maisha yake ikiwamo kupata ulemavu hata kifo.
“Takwimu za kidunia zinaonyesha mtu mmoja kati ya watu 10,000 ana tatizo la Himofilia, na Tanzania inakadiliwa kuwa na watu takribani milioni 67, hivyo inaweza kuwa na wagonjwa 6,700 hadi 13,000 na mpaka sasa wagonjwa waliobainika hapa nchini ni 631 na wanaendelea na matibabu,” amesema Makala.
Amesema, mtu mwenye Himofilia ataishi na ugonjwa huo maisha yake yote, lakini tatizo la kutokwa damu mfululizo hutibwa, ambapo gharama zake kwa mtu mmoja kwa mwaka mzima hutumia sh. milioni 243, na kwamba kwa mwaka jana pekee wamepokea dawa zenye thamani ya sh. bilioni 120 kutoka kwa wafadhili, Shirikisho la Himofilia Duniani.
Aidha, amesema katika Mkoa wa Shinyanga wameamua kuzindua Kliniki hiyo, ili kusogeza huduma kwa wananchi wenye matatizo hao na kupata tiba, sababu ugonjwa huo usipowahi kupata huduma mapema husababisha ulemavu na hata kifo.
Amesema, mbali na kuzindua Kliniki hiyo wametoa mafunzo kwa watalaamu wa afya jinsi ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa Himofilia katika Hospitali hiyo, kutoa vitendanishi vya maabara, vifaa vya mazoezi ya viungo, friji kwa ajili ya kutunzia dawa, kompyuta za kutunzia kumbukumbu za wagonjwa, na vitendea kazi vingine.
“nachukua fursa hii kuishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na Wizara ya afya kwa kuwapa mazingira bora wafadhili wetu Novo Nordisk, Himofilia na Haemoghlobinopathies Foundantion na Hospitali ya Taifa Muhimbili na chama cha Himofilia Tanzania kuboresha huduma hizi kwa wagonjwa wa damu,” amesema Makala.
Naye Neema Nicolaus mkazi wa Shinyanga, ambaye ana mtoto mwenye tatizo la Himofilia, amesema awali kabla ya kupata elimu juu ya ugonjwa huo, alimpeleka mtoto wake kwa waganga wa tiba za asili akiamini kuwa ni Imani za kishirikina, hali iliyosababisha mtoto wake kupata ulemavu.
Amesema, baada ya kupata uelewa, mtoto wake alimpeleka hospitali, na kubainika ana tatizo la Himofilia na siyo kurogwa, ndipo akapewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Kanda Bugando, huku akishukuru huduma hiyo ya tiba kuanza kutolewa Hospitali ya Rufaa Shinyanga.
Naye Rejina Shirima, ameiomba serikali ya Tanzania kuwekeza kwenye tiba ya dawa katika ugonjwa huo, ambapo dawa zake zina gharama kubwa, na kwamba siku wafadhili wakiondoka watakosa huduma hiyo na kuhatarisha maisha yao.
Naye Mganga wa Tiba Asili Mabula Joseph, amesema kwa elimu ambayo wamepewa juu ya ugonjwa huo wa Himofilia, hawatakaa tena na wagonjwa wa aina hiyo, bali watawashauri kwenda hospitali kwenye tiba sahihi.
MAELEZO KATIKA PICHA👇👇
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Timothy Sosoma akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kliniki ya wagonjwa wa Himofilia katika Hospitali ya Rufaa mkoani humo.
Katibu wa Chama cha Himofilia Tanzania na msimamizi wa mradi Abdallah Makala, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kliniki ya wagonjwa wa Himofilia katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dk. Augustino Maufi akizungumza.
Uzinduzi wa Kliniki ya wagonjwa wa Himofilia ukiendelea katika Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.