` AMANI KWANZA: VIJANA WAASWA KUEPUKA TAMAA KUPATA MAFANIKIO HARAKA KWA NJIA ZISIZO HALALI

WANDAMAN HOTEL

AMANI KWANZA: VIJANA WAASWA KUEPUKA TAMAA KUPATA MAFANIKIO HARAKA KWA NJIA ZISIZO HALALI

Usafirishaji haramu wa binadamu umeendelea kuwa tishio kubwa katika jamii, ukichangia kwa kiasi kikubwa kuvuruga amani ya familia na kuongeza wimbi la umasikini miongoni mwa wananchi.

Vitendo hivyo vinavyojihusisha na kuwahamisha watu kinyume cha sheria mara nyingi huacha madhara makubwa ya kijamii, kiuchumi na kisaikolojia kwa waathirika pamoja na familia zao pia athari kwa taifa huku vijana wakiaswa kuacha tamaa .

Hayo yameelezwa na afisa sheria kutoka Tume ya kurekebisha sheria Tanzania  Richard Mdee ,amesema usafirishaji haramu wa binadamu si tu unawaathiri watu binafsi, bali pia unaligharimu taifa kwa ujumla,Serikali hulazimika kutumia rasilimali nyingi katika kukabiliana na mtandao huo wa uhalifu kwa kutumia  rasilimali ambazo zingeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Aidha, vitendo vya usafirishaji haramu wa binadamu vinakiuka moja kwa moja haki za msingi za binadamu, ikiwemo haki ya uhuru, usalama na heshima ya utu hali ambayo inaondoa upendo na utulivu na kuchochea vitendo vya uhalifu ambavyo vinaweza kuwakosesha watu amani.

Waathirika mara nyingi hujikuta wakiishi katika mazingira magumu, wakinyimwa haki zao na kulazimishwa kufanya kazi zisizo na staha wala malipo stahiki pia  usafirishaji haramu wa binadamu huchochea kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani katika jamii.

Watu wanaosafirishwa kinyume cha sheria hukosa uhuru wa kufanya maamuzi sahihi, jambo linaloweza kuwapelekea kuingia katika shughuli haramu ili kuendelea kuishi.

Vilevile, kusafirisha mtu kwenda nje ya nchi bila kufuata taratibu za kisheria na kupitia mamlaka husika ni kosa linaloihujumu nchi,hatua hiyo si tu inakiuka sheria za nchi, bali pia inaathiri taswira ya taifa kimataifa na kuhatarisha usalama wa raia wake.

Kutokana na hali hiyo, vijana wameaswa kuepuka tamaa ya kupata mafanikio ya haraka kwa njia zisizo halali, badala yake, wanapaswa kujikita katika kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia sheria za nchi ili kujijengea maisha bora na ya heshima.

Imesisitizwa kuwa hakuna utajiri wa haraka unaopatikana bila juhudi halali, na kwamba mafanikio ya kweli yanahitaji uvumilivu, nidhamu na kujituma huku vijana wanahimizwa kushikamana, kudumisha utu na kuendeleza misingi ya amani, kwani hizo ndizo nguzo muhimu za maendeleo ya taifa lolote.

  

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464