
Ofisa Sheria wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Yosia Kimweri, amesisitiza umuhimu wa tume hiyo kupendekeza jeshi hilo kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya sheria, kanuni, na miongozo bila kujiingiza katika masuala ya kisiasa.
Kimweri amebainisha kuwa imani ya wananchi kwa jeshi hilo imeyumba kutokana na dhana ya polisi kuingilia siasa, hivyo ameshauri kuwepo kwa mikakati ya majadiliano na ushirikishwaji wa wazi ili jamii ilione jeshi hilo kama sehemu ya ulinzi.
Naye Mhadhiri kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Zacharia Swedi, amebainisha kuwa kuna haja ya kuwa na mwongozo wa wazi wa namna vyombo vya ulinzi vinavyopaswa kukabili hali za dharura kama zilizojitokeza wakati wa uchaguzi. Amesema kuwa muundo wa jeshi unapaswa kujali hali za watu na kulinda usalama wa raia ambao ulionekana kuwa hatarini.
Hoja nyingine nzito iliyoibuliwa ni hitaji la elimu kwa umma kuhusu madhara ya uharibifu wa mali za watu binafsi na miundombinu ya serikali, kama vile kuchomwa kwa vituo vya usafiri wa haraka (mwendokasi), jambo ambalo lilileta hasara kubwa kwa taifa.
Swedi amefafanua kuwa elimu hiyo ni muhimu ili wananchi waelewe wajibu wao katika kulinda amani na rasilimali za nchi hata nyakati za mivutano ya kisiasa.
Kwa upande wake, Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Musa Pambeje, ameshauri kuwepo kwa mfumo huru wa uchunguzi wa malalamiko dhidi ya polisi ili askari wanaokiuka sheria wawajibishwe, jambo ambalo litarejesha nidhamu na uaminifu ndani ya jeshi.
Aidha amehimiza matumizi ya teknolojia ya kisasa na uwazi katika operesheni za kiusalama kama njia ya kuondoa upotoshaji wa habari na kujenga imani kwa wananchi.
Pambeje amesisitiza kuwa jeshi linapofanya kazi kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati, linaziba mianya ya uvumi inayoweza kuchochea vurugu zaidi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464