
Wakati baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wakiendeleza chokochoko na kudai kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) haijafanya kitu, ukweli wa mambo unazidi kuumbua kashfa hizo kupitia takwimu na uwekezaji wa kimataifa.
Dunia sasa imeamua kuipigia saluti Tanzania, si kwa maneno matupu, bali kwa kuweka kambi ya uwekezaji katika sekta nyeti ya afya, ikiongozwa na imani kubwa kwa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye sasa anatazamwa kama kioo cha maendeleo ya kijamii barani Afrika.
Uthibitisho wa hili umejidhihirisha hivi karibuni Ikulu ya Dar es Salaam, kufuatia ugeni mzito kutoka taasisi ya kimataifa ya Keep a Child Alive (KCA) iliyoanzishwa na msanii nguli wa Marekani, Alicia Keys.
Ugeni huu uliolenga kuimarisha huduma za uzazi, umeweka msingi wa ujenzi wa wodi 27 za kisasa za kulelea watoto njiti nchini kote, hatua inayothibitisha kuwa Ilani ya CCM inatekelezwa kwa viwango vya kidunia huku ikichochea uwekezaji wa teknolojia ya hali ya juu na mafunzo kwa wataalamu wetu wa ndani.
Kwa upande wa takwimu, mafanikio haya yanaziba midomo ya wakosoaji kwani Tanzania imepiga hatua ya kihistoria kwa kupunguza vifo vya uzazi kutoka 556 mwaka 2016 hadi vifo 104 tu kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022.

Hali kadhalika, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kwa asilimia 36, jambo ambalo limeungwa mkono na Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia kwa Dkt. Mohamed Janabi, akisisitiza kuwa uwekezaji huu ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya serikali kuokoa maisha ya Watanzania.
Hoja inayopigwa mtandaoni kuwa maendeleo ni ya mjini pekee imejibiwa kwa vitendo kupitia uzinduzi wa jengo la kisasa la kuhudumia watoto njiti katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Rais Samia amebainisha kuwa mkakati wa serikali ni kujenga wodi 15 katika hospitali za mikoa na nyingine 20 katika hospitali za wilaya, lengo likiwa ni kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi jirani na makazi yao, huku kukiwa na ongezeko la ajira kwa watumishi wa afya na upatikanaji wa dawa za uhakika.
Heshima ya Tanzania imepaa kiasi kwamba Rais Samia sasa ndiye Kinara wa Umoja wa Afrika (AU) katika masuala ya afya ya uzazi, mama na mtoto, huku ziara ya Rais wa Ghana, John Dramani Mahama mkoani Arusha ikizidi kuimarisha diplomasia yetu.
Ni wazi kuwa mwelekeo wa sasa wa serikali si tu unaleta heshima kimataifa, bali unajibu kero za msingi za wananchi kwa vitendo, jambo linalofanya chokochoko za mitandaoni kukosa mashiko mbele ya ukweli wa huduma zinazotolewa hospitalini.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464