` WANANCHI SHINYANGA WATAKIWA KUPINGA RUSHWA KWA USHIRIKIANO

WANDAMAN HOTEL

WANANCHI SHINYANGA WATAKIWA KUPINGA RUSHWA KWA USHIRIKIANO

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Sunday Mtatiro,akizungumza na wananchi.

Na 

                                              Estomine Henry

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Sunday Mtatiro, amewataka wananchi kuongeza ushirikiano na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kuimarisha haki na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Akizungumza Machi 19, 2026 katika hafla ya futari (Iftar) iliyoandaliwa na TAKUKURU mkoani Shinyanga, Mtatiro alisema mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kufanikiwa bila ushiriki wa wananchi.

Alisema rushwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo na husababisha upotevu wa rasilimali za taifa, huku akibainisha kuwa vitendo hivyo vinahusisha pande zote mbili—wanaotoa na wanaopokea.

Mapambano ya rushwa yanahitaji ushirikiano wa dhati kutoka kwa wananchi ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinasimamiwa kwa uadilifu na kunufaisha wote,” amesema Mtatiro.

Aidha, alieleza kuwa changamoto ya ukosefu wa maadili kwa baadhi ya watumishi wa umma imekuwa ikichangia kuwepo kwa vitendo vya rushwa, hali inayosababisha wananchi kunyimwa haki zao.

Mtatiro aliwataka wananchi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa TAKUKURU, akisisitiza kuwa taasisi hiyo imejipanga kupokea na kufanyia kazi taarifa hizo kwa ufanisi.

“Mashauri mengi ya kesi yanaonesha wazi kuwa kuna upotoshaji wa ukweli kwa ajili ya kupata au kutoa rushwa ili kujinufaisha binafsi kwa kumdhulumu mwingine,” amesema Mtatiro

Mtatiro alipongeza TAKUKURU kwa kuendelea kutoa elimu kwa umma na kufanikisha ushiriki mkubwa wa wananchi katika hafla hiyo, akisema ni ishara kuwa jamii imeanza kuelewa umuhimu wa kupinga rushwa.Pia alieleza juhudi mbalimbali za maendeleo zinazoendelea kutekelezwa wilayani humo, hususan katika sekta ya afya, na kusisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa watumishi wa umma.

Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa ShinyangaDonnasian Kessy, alitoa zawadi kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu, akisema hatua hiyo inalenga kuimarisha mahusiano kati ya taasisi hiyo na jamii.

 Kessy aliwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kudhibiti vitendo hivyo vinavyokwamisha maendeleo.

                                                  








Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464