.jpg)
Katika kile kinachoonekana kuwa ni mkakati mzito wa kurejesha tunu za utaifa na kulinda mafanikio ya serikali, Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba ametoa agizo kali kwa wadau wa elimu kwa umma (washitiri) kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kutoa elimu ya uzalendo kwa Watanzania.
Akifungua Mkutano wa 110 wa Washitiri jijini Arusha ulioshirikisha taasisi 23 za umma, Dk. Mwigulu amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mmoja kusema na kutangaza mazuri yanayofanywa na serikali ili wananchi waweze kufurahia matunda ya kodi zao.Msisitizo huu unakuja wakati ambapo nchi inahitimisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya miaka 25 (2000-2025) mwezi Juni mwaka huu, jambo linalofanya tathmini ya mafanikio hayo kuwa hitaji la lazima kwa ustawi wa jamii.
Dk. Mwigulu ametoa onyo kali dhidi ya uholela na mifarakano ambayo imekuwa chanzo cha machafuko katika mataifa mbalimbali ya Afrika na nje ya bara hili, akibainisha kuwa kiini cha mivutano hiyo ni kupotea kwa uzalendo.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, kila Mtanzania ana wajibu wa kisheria na kimaadili kulinda rasilimali za nchi bila kujali itikadi za vyama, dini, wala ukabila.
Amewataka washitiri kuandaa maudhui yanayobeba ajenda za kitaifa ili kuziba mianya ya upotoshaji ambayo mara nyingi hutumika kama silaha ya kubomoa misingi ya amani na mshikamano iliyojengwa kwa miongo mingi nchini Tanzania.
Moja ya maeneo nyeti yaliyoguswa na Dk. Mwigulu ni matumizi mabaya ya vijana na teknolojia, ambapo ameeleza kusikitishwa na namna baadhi ya vijana wanavyotumika kuihujumu nchi kwa kuwasaidia wageni kumiliki rasilimali za wazawa au kukwepa kodi.
Alifananisha hali hiyo na usaliti wa harakati za uhuru, akihoji ingekuwaje kama vijana wa sasa wangekuwa katika mapambano ya kuiondoa ukoloni huku wakiwa na tabia ya kuwahifadhi watu wasio raia kwa maslahi binafsi.
Waziri Mkuu ametoa mwito kwa vijana kugeuka na kuwa walinzi wa rasilimali za taifa badala ya kuwa mawakala wa hujuma zinazolenga kuliangamiza taifa katika karne hii ya teknolojia.
Ili kukabiliana na mawimbi ya upotoshaji katika ulimwengu wa kidijitali, Dk. Mwigulu ameliagiza Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kujikita kikamilifu katika mitandao ya kijamii ambako ndiko kundi kubwa la vijana liliko.
Amesema kuwa serikali imejipanga kuongeza bajeti ya shirika hilo ili kuhakikisha usikivu wake unafika nchi nzima kwa asilimia 100 kutoka asilimia 87 ya sasa.
Lengo ni kuhakikisha kuwa habari sahihi za miradi ya maendeleo na mafanikio ya serikali zinawafikia wananchi kila pembe ya nchi na mtandaoni, badala ya kuwaacha vijana wakilishwa habari za uzushi na upotoshaji ambazo hazina tija kwa taifa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464