Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Wananchi wa Manispaa ya Shinyanga wamejadili na kutoa maoni rasimu ya mkataba wa huduma kwa wateja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), wakisisitiza kuendelea kutolewa kwa huduma bora ya maji, pamoja na kufungwa kwa mita za malipo ya kabla ili kudhibiti tatizo la malalamiko ya bili za maji.
Maoni hayo yametolewa leo Machi 26, 2026 katika mkutano wa wadau wa maji, uliolenga kujadili rasimu ya mkataba huo wa huduma kwa wateja.
Mmoja wa wananchi hao Ashirafu Said, amesema licha ya juhudi zinazofanywa na SHUWASA katika kuboresha huduma ya maji, bado kuna haja ya kuanzishwa kwa mita za malipo ya kabla ili kuondoa malalamiko ya wananchi kudai bili kubwa za maji.
“Tunawaomba SHUWASA muendelee kutoa huduma bora kwa wateja wenu, lakini ili kuondoa malalamiko ya bili kubwa za maji, tuwekeeni mita za malipo ya kabla kama ilivyo kwenye umeme wa ruku, tokeni zikiisha maji yanakata,” amesema Ashirafu.
Naye Mgeni rasmi Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, amewataka Shuwasa kwamba utoaji wao wa huduma uzingatie mkataba wa huduma kwa wateja na miongozi ya kisheria, kwa kutoa huduma bora ya maji kwa wananchi na kushughulikia matatizo au kero zao kwa wakati.
Awali, Mkurugenzi wa Shuwasa Mhandisi Yusuph Katopola, amesema mkataba wa huduma kwa wateja uliokuwepo umeisha, na sasa wapo kwenye kujadili rasimu ya mkataba mwingine ambao utadumu kwa muda wa miaka mitatu kuanzia 2026 hadi 2029 na utatumika mara baada ya kupitishwa na Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na Maji. EWURA.
Amesema mkataba huo una umuhimu mkubwa, kwa kuwa unaweka bayana haki na wajibu wa pande zote mbili, mtoa huduma na mteja, kwa lengo la kuongeza uwazi, uwajibikaji na kujenga uhusiano imara.
Aidha, amesema ufungwa wa mita za malipo ya kabla, utafanyika kwa hatua sababu zina gharama kubwa ikilinganishwa na mita za kawaida, na kwamba mita hizo wataanza kuzifunga kwanza kwenye maeneo ambayo yanachangamoto za ulipaji bili za maji hasa kwenye vituo vya umma vya kuchotea maji na zoezi hilo wanatarajia kuzifunga mwenzi April mwaka huu.
Naye Mkurugenzi wa huduma kwa wateja kutoka SHUWASA Rueben Mwandumbya, akiwasilisha wasilisho la mkataba wa huduma kwa wateja, ametaja majukumu ya mamlaka hiyo kwa wateja, kuwa ni kutoa huduma ya majisafi na salama yanayotosheleza katika viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa, kutoa huduma ya usafi wa mazingira kwa viwango vya juu, kuenga mahusiano mazuri na wateja.
Wajibu mwingine ni kulinda na kutunza mali na vyanzo vya maji, kutoa elimu kwa wateja juu ya sera ya taifa ya maji, kuwahamasisha wateja kulipa ankra za maji za kila mwezi kwa wakati na kulipa madeni ya maji, kupokea na kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa changamoto au malalamiko ya wateja, kukagua na kudhibiti uvujaji wa maji na kutunza kumbukumbu za wateja.
Ameongeza, pia kutoa maendeleo ya uendeshaji wa shughuli za mamlaka kwa wateja na umma kwa ujumla, kupendekeza bei za utoaji wa huduma za majisafi na majitaka kulingana na gharama za uendeshaji na kwa kuzingatia hali ya uchumi wa wateja, kumshirikisha mteja pindi zoezi la usomaji wa dira linapofanyika ili aweze kujua matumizi yake.
Haki za Mamlaka.
Ametaja haki za mamlaka kuwa ni kulipwa ankra za huduma ya majisafi na usafi wa mazingira, kulipwa malipo halali kutokana na huduma inayotolewa kwa mteja, kusitisha huduma ya maji kwa mteja asiyelipa kwa wakati ankra za maji ndani ya siku 30, kuchukua hatua za kisheria kwa waharibifu wa miundombinu pamoja na wezi wa maji.
Wajibu wa mteja kwa Mamlaka
Kulipa ankra za maji kwa wakati, kutoa ushirikiano kwa watumishi wa mamlaka wanapowahudumia, kutoa taarifa sahihi za rushwa, wizi wa maji na uharibifu wa mali za mamlaka, kulinda na kutunza vyanzo vya maji, na kuhudhuria mikutano inayoitishwa na mamlaka ili kupata taarifa mbalimbali.
MAELEZO KATIKA PICHA👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo akizungumza.
Mkurugenzi wa Shuwasa Mhandisi Yusuph Katopola akizungumza.
Mkurugenzi wa huduma kwa wateja kutoka SHUWASA Rueben Mwandumbya akiwasilisha mkataba wa huduma kwa wateja.
Mwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya SHUWASA Ruben Kitinya akizungumza.