` UKATILI WAELEZWA KUWA KIKWAZO KWA MAENDELEO YA UCHUMI

WANDAMAN HOTEL

UKATILI WAELEZWA KUWA KIKWAZO KWA MAENDELEO YA UCHUMI

Ukatili wa kijinsia umeendelea kuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo nchini kwani unadumaza nguvu kazi na kurudisha nyuma juhudi za kujenga taifa lenye usawa. 

Vitendo kama ukeketaji, ndoa za utotoni, na mila kandamizi si tu kwamba vinakiuka haki za binadamu, bali vinasababisha mmomonyoko wa maadili na kukosekana kwa amani ndani ya familia. 

Athari hizi zinatengeneza mnyororo wa umaskini ambao unalizuia taifa kufikia malengo yake ya kiuchumi, kwani jamii iliyojawa na hofu na ukatili haiwezi kuwa na tija katika uzalishaji wala kushikamana katika ujenzi wa nchi.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua Mradi wa PAMOJA wenye thamani ya Shilingi bilioni 262 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, unaolenga mikoa 10 na halmashauri 40 nchini. 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima, amebainisha kuwa mradi huu ni silaha kubwa katika kukuza usawa na kutokomeza ukatili wa kijinsia ifikapo mwaka 2030.

 Lengo kuu ni kuhakikisha wanawake wanaimarika kiuchumi kupitia Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi (TUMAUWAKI), hatua inayokwenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kujenga jamii yenye neema na usawa.

Mikakati ya utekelezaji wa mradi huu inajumuisha uimarishaji wa miundombinu ya ustawi wa jamii ambapo vituo 200 vya kulea watoto vitajengwa ili kumpa mwanamke nafasi ya kushiriki shughuli za kiuchumi kwa uhuru. 

Aidha, serikali imepanga kujenga nyumba salama 10 kwa ajili ya waathirika wa ukatili pamoja na ofisi 40 za maendeleo ya jamii ili kusogeza huduma karibu na wananchi. Mpango huu unatoa kipaumbele pia katika kutoa mikopo yenye masharti nafuu maeneo ya vijijini na kutoa elimu kwa wanaume na jamii kwa ujumla ili kupinga mila potofu na ukatili, jambo ambalo ni msingi wa kujenga familia bora na salama.

Imeelezwea kuwa azma ya mradi huo si kudidimiza wanaume, bali ni kuwashirikisha kama nguzo muhimu katika ujenzi wa familia zenye upendo na hekima. 

Naibu Waziri kutoka Zanzibar, Zawadi Amour Nassour, amesisitiza kuwa uwepo wa familia bora ndio chimbuko la taifa endelevu na lenye furaha.

 Kupitia usimamizi madhubuti wa sekreterieti ya mradi na ushirikiano wa viongozi wa mikoa kama Geita, serikali ina matarajio makubwa ya kuona vitendo vya ukatili vinalimalizika kabisa, huku ikimwacha mwanamke wa Kitanzania akiwa na uchumi imara na hadhi inayostahili ndani ya jamii iliyoshikamana. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464