Na Estomine Henry-Shinyanga.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilaya ya Shinyanga umewakaribisha wadau kutoka ndani na nje ya mkoa huo kuwekeza katika Msitu wa Lubaga kwa ajili ya kuendeleza utalii wa endelevu.
Akizungumza na vyombo vya habari wakati wa maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka Machi 21, Ofisa Mwandamizi wa Uhifadhi kutoka TFS Wilaya ya Shinyanga .Fabian Balele, alisema kuwa miradi ya ujenzi wa hoteli, kumbi za mikutano na viwanja vya michezo imepewa kipaumbele ili kufungua fursa kwa jamii kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Balele alieleza kuwa TFS imeandaa mipango madhubuti ya uwekezaji itakayoshirikisha wadau mbalimbali wenye nia ya kuwekeza katika miradi ya kiuchumi ndani ya msitu huo.
“Hii ni fursa adhimu kwa Watanzania kuwekeza na kujipatia vyanzo vya mapato kupitia rasilimali za misitu huku tukilinda mazingira,” alisema Balele.
Aliongeza kuwa tayari kuna jitihada za kuendeleza miundombinu na vivutio mbalimbali ili kuboresha mazingira ya mapumziko na kuwezesha shughuli za kijamii kama vile harusi, mahafali na mikutano ya vikundi kufanyika katika eneo hilo.
“Aidha, aliwahimiza wawekezaji kujitokeza kwa wingi, akisisitiza kuwa TFS iko tayari kuingia mikataba ya ushirikiano na wadau wote watakaokuwa tayari kuwekeza.amesema Balele
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kamanda wa TFS Kanda ya Magharibi ambaye pia ni Afisa Misitu Mwandamizi na Mkuu wa Operesheni Kanda, Shadrack Msilu, aliwataka wadau kutumia fursa zilizopo katika misitu ya mikoa ya Katavi, Shinyanga, Kigoma na Tabora kwa ajili ya uwekezaji.
Msilu alibainisha kuwa katika mkoa wa Shinyanga kuna misitu ya asili ya Ngitili, hususan katika maeneo ya Mhunze-Kishapu, ambako kuna fursa kubwa za biashara, ikiwemo kuanzisha kambi maalum za huduma kama vile nyama choma wakati wa minada inayovutia watu wengi.
“Iwapo wadau wako tayari, tutatoa maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji huo ili kuboresha huduma na kuongeza thamani ya kiuchumi katika maeneo hayo,” amsema Msilu.
Waandishi wa habari waliofika katika eneo hilo walipongeza juhudi za TFS katika kuendeleza miradi ya kimkakati ndani ya misitu hiyo, wakieleza kuwa hatua hiyo itaongeza vivutio vya utalii na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Shinyanga.
MAELEZO KATIKA PICHA👇👇
Ofisa Mwandamizi wa Uhifadhi kutoka TFS Wilaya ya Shinyanga Fabian Balele akizungumza.
Ofisa Mwandamizi wa Uhifadhi kutoka TFS Wilaya ya Shinyanga Fabian Balele akizungumza.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464