` TANZANIA NA ATIDI KUPUNGUZA VIHATARISHI VYA UWEKEZAJI

WANDAMAN HOTEL

TANZANIA NA ATIDI KUPUNGUZA VIHATARISHI VYA UWEKEZAJI

Serikali ya Tanzania imedhamiria kuimarisha ushirikiano wake na Shirika la Bima ya Maendeleo ya Biashara na Uwekezaji Afrika (ATIDI) ili kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia mitaji zaidi kutoka sekta binafsi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.
Hatua hiyo inakuja wakati taifa likiweka msisitizo katika kupunguza vihatarishi vya uwekezaji ili kuwapa ujasiri wawekezaji na taasisi za kifedha kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amebainisha hayo jijini Dar es Salaam wakati wa warsha maalum ya ATIDI kuhusu kuimarisha mazingira ya biashara nchini iliyofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Omar alilipongeza shirika hilo kwa mchango wake wa kipekee katika kutoa huduma za kupunguza hatari za uwekezaji (de-risking), jambo ambalo limekuwa chachu ya mafanikio kwa miradi mingi barani Afrika.

Balozi Omar alieleza kuwa Tanzania inajivunia kuwa miongoni mwa wanachama waanzilishi wa ATIDI, chombo kilichoundwa mahususi kutoa suluhisho za Kiafrika kwa changamoto zinazolikabili bara hili.

Alifafanua kuwa licha ya Afrika kuwa na fursa nyingi za uwekezaji, imekuwa ikikabiliwa na mtazamo hasi kuhusu hatari za mikopo, hali iliyofanya uwepo wa shirika kama ATIDI kuwa hitaji muhimu katika kurejesha imani ya wawekezaji kwenye sekta za miundombinu, viwanda na nishati.

Katika takwimu zilizowasilishwa, ilielezwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazonufaika zaidi na huduma za shirika hilo, ikiwa tayari imeshuhudia miradi yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 7.8 ikitekelezwa kwa ushirikiano huo. Miradi hiyo inajumuisha sehemu ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), jambo linalothibitisha kuwa ushirikiano huo unakwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 inayolenga kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi.

Dira ya 2050 inalengo la kuifanya Tanzania kufikia hadhi ya uchumi wa kipato cha juu na kuongeza Pato la Taifa (GDP) mara kumi zaidi. Ili kufanikisha azma hiyo, Balozi Omar alisisitiza umuhimu wa kuwa na uratibu imara katika sekta ya fedha na taasisi zinazosaidia kupunguza hatari za kibiashara. Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuweka sera rafiki za kodi na mazingira wezeshi ili kuhakikisha sekta binafsi inakuwa injini kuu ya ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ATIDI, Bw. Manuel Moses, aliahidi kuwa taasisi yake itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuchochea mitaji zaidi kuingia nchini. Alibainisha kuwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001, ATIDI imekua na kuwa mtoa huduma mkubwa wa bima ya uwekezaji Afrika, ikisaidia biashara zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 93 katika nchi mbalimbali barani humu.

Nchini Tanzania, mchango wa ATIDI umegusa maeneo mengi ya kimkakati yakiwemo miundombinu ya viwanja vya ndege, barabara, madaraja, na miradi ya nishati inayoratibiwa na TANESCO pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Aidha, shirika hilo limekuwa likiunga mkono taasisi za kifedha na biashara ndogo na za kati (SMEs), mbali na kufadhili miradi ya kijamii kama ule wa uthabiti wa Gridi ya Taifa na usafi wa mazingira.

Shirika la ATIDI, ambalo zamani lilijulikana kama African Trade Insurance Agency (ATI), linaendelea kuwa kiungo muhimu katika kupunguza hatari za uwekezaji na kutoa dhamana za biashara. Kwa kuimarisha ushirikiano huu, Tanzania inajipanga vyema kutumia fursa zilizopo ndani ya mipaka yake na katika ukanda mzima wa Afrika ili kuhakikisha maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464