Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI inaendelea kusimamia uboreshwaji wa miundombinu ya elimu nchini, ili kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata haki yake ya msingi ya elimu bora katika mazingira mazuri na rafiki ya ujifunzaji na ufundishwaji.
Prof. Shemdoe amesema, kukamilika kwa ujenzi wa Shule ya Msingi iliyopewa jina la Profesa Riziki Shemdoe ni sehemu ya utekelezaji wa azma hiyo ya Serikali ya kumuwezesha mtoto wa kitanzania kupata haki yake ya msingi ya elimu bora.
Prof. Shemdoe amesema hayo leo Machi 22, 2026 akiwa katika Kata ya Ngwelo wilayani Lushoto, mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika Shule hiyo Mpya ya Awali na Msingi ya Profesa Riziki Shemdoe iliyojengwa katika Jimbo la Lushoto, Tarafa ya Mlola, Kata ya Ngwelo, Kijiji cha Kihitu.
Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, ujenzi wa shule hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala Chama Cha Mapinduzi pamoja na maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mtoto aliyefikisha umri wa kwenda shule anapata haki ya elimu kwa kuboreshewa mazingira bora na rafiki ya ujifunzaji.
Akizungumzia chimbuko la wananchi kuipa shule hiyo Jina Lake, Prof. Shemdoe amesema eneo hilo lililojengwa shule hiyo lilitolewa na baadhi ya wananchi kwa sharti la kupewa eneo lingine watakaloendelea na shughuli zao za kilimo, ndipo kwa pamoja familia ya Marehemu Mzee Silas Joseph Shemdoe iliamua kuwapatia wananchi hao shamba ili kupisha ujenzi wa shule hiyo.
Msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa Shule hiyo Bw. Mohamed Mtumbuka, amesema shule hiyo ndio mradi pekee wenye majengo ya kisasa zaidi katika Kata ya Ngwelo, ambao Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza fedha ili kuboresha miundombinu ya kuwawezesha wanafunzi kupata ufaulu mzuri.
Naye, Mkazi wa Kata ya Ngwelo Bw. Ramadhan Saguti amesema kupitia ujenzi wa shule hiyo wananchi wa kata hiyo wameanza kulipata tabasamu lililoahidiwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuongeza kuwa wanaendelea kumuombea ili aendelee kuwapatia tabasamu.
Akifurahia shule hiyo kujengwa, Mwanakombo Idrisa ambaye ni mmoja wa Wanafunzi wa Shule Mama ya Msingi Ngwelo anayetarajia kuhamia katika shule mpya ya Profesa Riziki Shemdoe, ametoa ahadi kwa Mhe. Rais kuwa hato muangusha na atahakikisha atasoma kwa bidii ili apate ufaulu mzuri utakaoendana miundombinu bora ya shule iliyojengwa.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule wa Shule ya Msingi Profesa Riziki Shemdoe, Bw. Riziki Mwanyoka amemsukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga shule iliyowaletea tabasamu wananchi wa Kijiji cha Kihitu na kumuahidi kwamba atahakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na ufaulu mzuri.


