` PETRONILA MWANAGENZI MSICHANA ANAYEPELEKA MAPINDUZI YA MUSULI UFUNDI MAGARI

WANDAMAN HOTEL

PETRONILA MWANAGENZI MSICHANA ANAYEPELEKA MAPINDUZI YA MUSULI UFUNDI MAGARI

Katika ulimwengu ambao bado unawaona mabinti wakiwa wamekaa ofisini na majalada ya sheria au makaratasi ya uhasibu, au kujiegemeza kwa wanaume, Petronila Thobias Peter ameamua kuchora ramani yake tofauti. 

Baada ya kuhitimu masomo yake ya Kidato cha Sita, mwelekeo wa maisha yake ulikuwa umeshaandaliwa na matamanio ya baba yake—uanasheria.

Lakini ndani ya moyo wa Petronila, hakukuwa na sauti ya mahakama wala majoho meusi. Kulikuwa na mngurumo wa injini na harufu ya grisi.

“Muda wote hamu yangu ilikuwa kufanya kazi zenye pilikapilika, kazi zinazotumia musuli na zinazoleta matokeo ya kuonekana kwa macho,” anasema Petronila, huku macho yake yaking’aa kwa ujasiri wakati wa mahojiano na timu ya Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Ajira na Mahusiano) waliofika katika eneo analochukulia mafunzo ya uanagenzi,  Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Singida (Singida FDC) . 

Kwake, urembo haukuwa kwenye kucha zilizopakwa rangi, bali kwenye mikono iliyojaa madoa ya mafuta ya injini ambayo yanashuhudia ufundi na akili kubwa.

Petronila anasema bahati ilimwangukia aliposikia tangazo la programu ya uanagenzi inayoendeshwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano). Bila kusita, alizungumza na baba yake ambaye aliridhia aachane na matarajio ya uanasheria na kujiunga na Chuo  CHA Singida FDC kujifunza ufundi. 

Alifanikiwa katika usaili na leo hii, Petronila ni mmoja wa vijana 5,746 nchi nzima wanaonufaika na programu hii, akijifunza kwa miezi minane—sita ya nadharia na miwili ya mafunzo kwa vitendo (field).

Ndani ya muda mfupi, binti huyu amekuwa gumzo chuoni hapo. Mwalimu wake wa idara ya ufundi magari, Ibrahim Salum Kitogo, anashindwa kuficha furaha yake. 

“Petronila ni miongoni mwa mabinti wanne tu kati ya wanafunzi 25 wanaojifunza ufundi magari kupitia programu hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Lakini spidi yake ya kuelewa injini na namna zinavyofanya kazi ni kubwa sana. Anafanya vyema mno,” anasema Mwalimu Kitogo.

Kila anaposhika spana, Petronila anamuona shujaa wake—mwanamke mmoja shupavu wa TANAPA ambaye si tu ni fundi mahiri, bali pia anamiliki gereji yake mwenyewe. Hilo ndilo lengo la Petronila. Hataki tu kuwa mfanyakazi; anataka kuwa mmiliki wa gereji, malkia wa mitambo atakayetoa ajira kwa wengine.

Hata hivyo, safari hii ina maono mapana zaidi. Petronila anaishukuru serikali kwa fursa hii ya uanagenzi inayowatoa vijana mitaani na kuwapa ujuzi wa maisha, lakini ana neno moja kwa watunga sera: “Mafunzo haya ni dhahabu, lakini baada ya hapa tunahitaji zana. Ikiwezekana, mhitimu anapomaliza, awezeshwe na mtaji au hata vifaa vya kazi (tool kit) ili tuanze kazi mara moja.”

Kwa Petronila, kazi ya ufundi magari si tu 'kazi ya kiume,' bali ni sanaa, ni sayansi, na ni uhuru wa kiuchumi. Anatoa wito kwa wasichana wote nchini Tanzania kuacha kuogopa kazi za musuli. Programu ya uanagenzi ni mlango wazi wa kujiokoa na vishawishi vya mitaani na kujenga maisha imara.

“Kwa nafasi niliyoipata, nitahakikisha naifanyia vyema. Wasichana wenzangu, msiogope mafuta ya injini. Huu ndio uwanja wetu mpya wa vita, na tunashinda,” anasema Petronila, binti aliyekataa sheria ili akatengeneze 'sheria' mpya kwenye injini za magari.

Chini ya kaulimbiu isemayo “Nguvukazi yenye Ujuzi Stahiki kwa Ajira Endelevu,” Serikali imeweka bayana dhamira yake ya kupunguza pengo la ujuzi linalowakabili vijana wengi nchini. Programu hii inalenga kuleta mabadiliko ya kifikra na kiuchumi kwa kutoa mafunzo yanayoakisi mahitaji halisi ya soko la ajira, yakijikita katika mchanganyiko wa nadharia na vitendo.

Uzinduzi wa awamu ya nane ya programu hii, umefanyika Machi 8 mwaka huu.Uendelevu wa programu unakuja wakati ambapo nchi inajipanga kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ikihitaji nguvukazi yenye ushindani wa kimataifa. 

Mafunzo hayo ya uanagenzi yapo katika fani mbalimbali ikiwamo ubunifu wa mitindo na ushonaji nguo,ufundi uashi,ufundi magari,ufundi umeme wa majumbani, uchomeleaji na uungaji vyuma, kilimo na mifugo,uendeshaji wa mitambo, mashine za kunyanyua mizigo na ufundi bomba  yanayotolewa kupitia vyuo 46 vilivyosambaa katika mikoa 25 ya Tanzania Bara, ambapo vyuo 29 ni vya Serikali na 17 ni vya sekta binafsi .

Programu hii ya uanagenzi ni sehemu ya mikakati ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano katika kuhakikisha kuwa nguvukazi ya Taifa inapata stadi muhimu za kuajirika au kujiajiri, hivyo kuchochea ukuaji jumuishi wa uchumi kuelekea mwaka 2050.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464