` MKANDARASI ANAYEJENGA BARABARA KUELEKEA UWANJA WA AFCON 2027 ARUSHA HATAONGEZEWA MUDA - PROF. SHEMDOE

WANDAMAN HOTEL

MKANDARASI ANAYEJENGA BARABARA KUELEKEA UWANJA WA AFCON 2027 ARUSHA HATAONGEZEWA MUDA - PROF. SHEMDOE

 

Na OWM - TAMISEMI, Arusha

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe ameitaka kampuni ya M/s China Railway Construction Engineering Group kuhakikisha ifikapo Mei 2027 iwe imekamilisha ujenzi wa miundombinu ya bababara za kuelekea na kuzunguka uwanja mpya utakaotumika katika Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, katika Jiji la Arusha, kwani hakutakuwa na nyongeza ya muda kwa mkandarasi huyo.

Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo kwa kampuni hiyo leo machi 20, 2026 jijini Arusha, mara baada ya kushuhudia Hafla ya Utiaji Saini Mkataba wa Uboreshaji wa Ujenzi wa Miundombinu ya Barabara za kuelekea na kuzunguka uwanja mpya wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) unaoendelea kujengwa katika jiji hilo.

“Mkandarasi, barabara hizi tulizosaini mikataba ya ujenzi wake leo zinatakiwa kukamilika Mei 2027 na hakutakuwa na muda wa nyongeza ya kukamilisha ujenzi wa wa barabara hizo,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia na kuidhinisha zaidi ya Shilingi Bilioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo, na kuongeza kuwa ni ukweli usiopingika kwamba barabara zinazojengwa na TARURA zina mchango mkubwa katika ukuaji wa ustawi wa uchumi kwani zinawagusa wananchi moja kwa moja. 

Naye, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini ambaye ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Paul Makonda ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI kwa kuleta fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi wa Jiji la Arusha, huku akiitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ya ujenzi wa Stendi ya Kisasa ya Mabasi, Ujenzi wa Soko, Ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano wa Jiji pamoja na Ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Jiji la Arusha.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff amesema kuwa sambamba na ujenzi wa uwanja huo wa AFCON, leo Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa Miundombinu muhimu ya barabara yenye jumla za kilomita 21.2 kwa kiwango cha lami kuelekea na kuzunguka uwanja wa AFCON, likiwepo na daraja moja (1) la upana wa Mita 100 ambalo litajengwa katika barabara ya Essuri.

Mhandisi Seff ameanisha kuwa, mradi huo wa ujenzi wa barabara kuelekea uwanja wa AFCON utagharimu kiasi cha Shilingi 82,908,500,000.00. ambapo kati ya fedha hizo, shilingi 81,500,250,000.00 ni gharama za usanifu wa kina na ujenzi kwa Mkandarasi na Shilingi 1,408,500,000 ni gharama za Mshauri Elekezi za usanifu wa awali na kutayarisha mahitaji ya Mwajiri.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464