` MAONO YA KIMKAKATI: SERIKALI INAVYOWEKEZA KWENYE GESI ASILIA KULETA USTAWI

MAONO YA KIMKAKATI: SERIKALI INAVYOWEKEZA KWENYE GESI ASILIA KULETA USTAWI

KATIKA jitihada za kuhakikisha Tanzania inakuwa na nishati ya kutosha na ya uhakika, Serikali ya Awamu ya Sita imetangaza kuwekeza kiasi cha Shilingi trilioni moja mkoani Mtwara kwa ajili ya miradi ya uchimbaji wa visima vya Ntorya na ujenzi wa bomba la gesi kuelekea Madimba. 

Uwekezaji huu mkubwa unalenga kuimarisha miundombinu ya gesi asilia, hatua inayotajwa kuwa mkombozi wa kiuchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, huku ikizingatia utunzaji wa mazingira.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi hiyo mkoani humo, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya maono mapana ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kutumia rasilimali za ndani kwa ajili ya ustawi wa wananchi. 

Waziri Ndejembi amebainisha kuwa hatua itakaongeza upatikanaji wa nishati kwa matumizi ya viwandani na majumbani.

Moja ya faida kuu ya mkakati huu ni kulinda mazingira kwa kutoa mbadala wa nishati safi. Kwa kuongeza uzalishaji wa gesi asilia, Serikali inalenga kupunguza utegemezi wa mkaa na kuni, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa misitu nchini. Hii ina maana kuwa, mwananchi hatapata tu umeme wa uhakika, bali pia atakuwa na uwezo wa kutumia nishati rafiki kwa mazingira itakayoboresha afya na hali ya hewa.

Katika kile kinachoonekana kama msisitizo wa nidhamu ya kazi, Waziri Ndejembi ametoa agizo kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuhakikisha kuwa ifikapo Septemba 2026, uzalishaji wa gesi katika eneo la Ntorya uanze rasmi. Ameonya kuwa Serikali haitavumilia ucheleweshaji wowote usio na tija, kwani lengo ni kuona matokeo ya uwekezaji huo yakigusa maisha ya Watanzania moja kwa moja bila visingizio.

Aidha, Serikali imeweka wazi kuwa uwekezaji huu ni sehemu ya mpango kabambe wa kuongeza uzalishaji wa umeme nchini kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030. Ongezeko hili la nishati linatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi, hasa katika Ukanda wa Kusini, kwa kuvutia wawekezaji wa viwanda na kutoa fursa za ajira kwa vijana wa Kitanzania.

Sambamba na maendeleo hayo ya kiufundi, Waziri amesisitiza umuhimu wa Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii (CSR). Ameielekeza TPDC kuhakikisha jamii inayozunguka miradi hiyo inanufaika kupitia miradi ya maendeleo itakayotekelezwa kwa ushirikiano na halmashauri husika. Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa rasilimali za taifa zinajenga mustakabali mwema wa elimu, afya, na miundombinu kwa wananchi wa maeneo hayo.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464