.jpg)
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepongezwa kwa kuandika historia baada ya kuidhinisha Shilingi Bilioni 335 kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kimkakati wa Bwawa la Kidunda, mkoani Morogoro, hatua itakayohitimisha kabisa adha ya maji kwa wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Pongezi hizo zimetolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, baada ya kutembelea mradi huo wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Mhe. Jackson Kiswaga (Mb).Mradi huo unatekelezwa kwa asilimia 100 kwa fedha za walipakodi wa Tanzania.
Mhe. Kiswaga amebainisha kuwa mradi huo ni jibu la kudumu dhidi ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi na ukame, akisisitiza kuwa Bunge litahakikisha linasimamia vyema utekelezaji wake ili kila senti iliyotolewa na Rais Samia ilete tija iliyokusudiwa kwa wakati.
Mradi wa Bwawa la Kidunda si tu mkombozi wa huduma ya maji, bali ni injini ya maendeleo itakayohusisha, hifadhi ya maji ya kiasi cha lita bilioni 190, hatua itakayohakikisha utulivu wa huduma hata nyakati za ukame mkali. Aidha kutakuwa na uzalishaji wa umeme kiasi cha megawati 20 zitakaosaidia kuchochea shughuli za kiuchumi.
Pia katika mradi huo kutakuwa na ujenzi wa barabara ya kilometa 75 kwa kiwango cha changarawe kutoka Ngerengere hadi Kijiji cha Kidunda, ikifungua fursa za usafirishaji na biashara.
Akitoa ripoti ya maendeleo ya mradi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, ameeleza kuwa ujenzi umefikia asilimia 47 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2026. Kasi hiyo imechangiwa na usimamizi madhubuti wa Wizara ya Maji, ambapo Naibu Katibu Mkuu, Rose Ambrose, amehakikisha kuwa vikwazo vyote vinatatuliwa ili mradi usikwame.
Utekelezaji wa mradi huu wa Kidunda ni ushahidi mwingine wa namna Rais Samia anavyopambana kuondoa kero za wananchi kwa vitendo, akihakikisha rasilimali za nchi zinatumika kujenga miundombinu itakayodumu kwa vizazi vijavyo na kuimarisha usalama wa maji nchini.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464