` KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YARIDHISHWA NA UTEKELEZWAJI MRADI WA KITUO CHA TAIFA CHA UTENGAMAO

WANDAMAN HOTEL

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YARIDHISHWA NA UTEKELEZWAJI MRADI WA KITUO CHA TAIFA CHA UTENGAMAO

 

Na; Mwandishi wetu - Dodoma.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imetembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Utengamao cha Taifa unaotekelezwa na Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) katika eneo la Itega, jijini Dodoma.

Ziara hiyo imefanyika leo tarehe 18 Machi 2026 na kuongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Edwin Swale (Mb) ikiwa ni sehemu ya majukumu ya kamati ya kusimamia na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Swale amesema kuwa kamati imeridhishwa na hatua ya utekelezaji  ambayo mradi umefikia kwani unaenda kutimiza  dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujali Utu na Ustawi wa Watanzania.

Sambamba na hilo, ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu kupitia Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za Kulevya kwa kubuni mbinu ya jinsi ya kusaidia waraibu watokanao na matumizi ya madawa za kulevya.

Awali,Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amesema kuwa Mradi huo ni endelevu ikiwa ni juhudi ya Serikali katika mapambano dhidi ya Dawa za kulevya na kuahidi kuendelea kushirikiana na Taasisi binafsi katika mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za kulevya Nchini.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya Bw. Aretas Lymo ameongeza kuwa kituo hiko kinatarajia kutoa huduma za matibabu, urekebishaji wa kitabia pamoja programu za kuwawezesha waathirika kurejea katika jamii wakiwa na uwezo wa kujitegemea.

Wakati huo huo, Makamu Mwenyekiti Mhe. Swale ameelekeza kuwa Ujenzi wa kituo hicho cha utengamao uzingatie Uwepo wa Miundombinu ya watu wenye mahitaji maalum na kutilia maanani malengo ya kituo ya kuwasaidia kiujuzi waraibu wa madawa ya kulevya.










Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464