Na Richard Bagolele, SHINYANGA
Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imepongezwa kwa usimamizi mzuri ya miradi ya kuimarisha na kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) na mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambapo imesababisha kuwa na shule bora na ya kisasa ya wasichana pamoja na kuanzisha shule mpya ya Amwali na Msingi ya Butulwa kupitia miradi hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa jana na timu ya ufuatiliaji wa pamoja kutoka Benki ya Dunia ambao ndio wafadhili wa miradi hiyo, Wizara ya Elimu pamoja na TAMISEMI waliofika kwa ajili ya ukaguzi wa miradi hiyo.
Wajumbe wa timu hiyo wamesema Manispaa ya Shinyanga imefanya vizuri katika hatua zote hadi kukamilika kwa ujenzi huo ambao vigezo vyote vilivyotolewa vimezingatiwa vyema hivyo wameipongeza Manispaa hiyo kwa jitihada hizo ambazo zimeifanya kuwa na shule nzuri ya mfano miongoni mwa shule 26 zilizojengwa nchini.
"Shule hizi mbili tulizozitembelea kwakweli zinavutia, hata wafadhili wetu wamefurahia kuona miundombinu mizuri hususan shule ya wasichana ya Shinyanga na tumeshuhudia kwa macho yetu mabweni mazuri, Maktaba nzuri, maabara ya kisasa kabisa hili limeifanya shule hii kuwa miongoni mwa shule bora kabisa nchini Tanzania" amesema DKt. Theresia Kuiwite kutoka TAMISEMI.
Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia Bi.Edinah Kashangati amesema kupitia ukaguzi huo Manispaa ya Shinyanga imejitahidi kutunza mazingira ya shule hiyo ikiwemo upandaji wa miti, upatikanaji wa umeme na maji ambavyo ni vigezo mhimu kutoka kwa mfadhili hivyo ameomba Manispaa kuitunza vizuri miundombinu hiyo iweze kudumu huku wakitoa sifa nyingi kwa Mkuu wa Shule hiyo Bi. Nura Kamumtu kwa usimamizi mzuri pamoja na mahusiano mazuri na wanafunzi na walimu wengine.
Katika hatua nyingine timu hiyo imempongeza Mkurugenzi wa Manispaa kwa kuhakikisha anasimamia vyema huduma mhimu hususan uwepo wa chumba cha wagonjwa pamoja na mtaalamu wa afya shuleni hapo ambapo amesema kuwepo kwa huduma hiyo kunaifanya shule hiyo kuwa shule bora na ya mfano nchini.
Kwa upande wake kaimu mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari maalumu Richard Makoye amesema ubora wa shule hiyo umechangiwa kutokana na ushirikiano mkubwa ulipo baina ya Manispaa na na idara ya Elimu, ambapo amesema kwa sasa shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma na kushika nafasi ya Kwanza kiwilaya na ya pili kimkoa kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha pili mwaka 2025.
Timu hiyo ya pamoja ya ufuatiliaji imetembelea Sekondari ya Wasichana ya Shinyanga iliyojengwa kupitia mradi wa SEQUIP kwa gharama za Shilingi Bilioni 4.3 pamoja na shule mpya ya awali na msingi ya Butulwa kwa gharama ya Shilingi milioni 342.9 kupitia mradi wa BOOST.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464










