Na Marco Maduhu, SHINYANGA
MKURUGENZI wa Shirika la Rafiki SDO Gerald Ng’ong’a, amezindua rasmi zoezi la ulaji wa chakula kwa wanafunzi shule ya msingi Iwelyangula Kata ya Kitangili manispaa ya Shinyanga, ili wasome kwa bidii na kufanya vizuri kitaaluma kwa kupata ufaulu wa juu.
Mbali na kuzindua ulaji huo wa chakula shuleni hapo, Ng’ong’a amekabidhi pia chakula kilo 900 za mahindi, kilo 145 za sukari na kilo 25 za unga.
Amezindua zoezi hilo leo Machi 4,2026, alipokuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, ambayo ngazi ya Manispaa ya Shinyanga, yamefanyika katika shule ya msingi Iwelyangula na kilele chake ni Machi 8..
Ng’ong’a amesema, utoaji wa chakula shuleni, kutamsaidia mwanafunzi kuzingatia masomo yao na kufanya vizuri kitaaluma, na kwamba mbali na kukabidhi chakula hicho, kila baada ya miezi mitatu atakuwa akitoa kila 100 za mahidi ili ulaji wa chakula uwe endelevu.
“Natoa wito kwa wazazi muunge juhudi hizi za uchangiaji wa chakula shuleni, ili wanafunzi wapate chakula, na leo tunazindua rasmi kwa vitendo ulaji wa chakula kwa wanafunzi hapa Iwelyangula na uwe endelevu ,tunawaomba wazazi mguswe na hili suala mtoto akisoma akiwa ameshiba atazingatia masomo na kufanya vizuri kitaaluma,” amesema Ng’ong’a.
Amesema, wao kama wadau wa maendeleo wanaguswa na suala la utoaji wa chakula shuleni, na ndiyo maana amewiwa na kuamua kutafuta wadau wengine pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga kuchangia chakula shuleni hapo, ili wanafunzi waanze kula chakula na kuinua ufaulu.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Iwelyangula Amina Madua, amemuunga mkono mdau huyo wa maendeleo, na kuahidi kwamba nayeye kila baada ya miezi mitatu atakuwa akitoa kilo 30 za mahidi, huku diwani wa Vitimaalum Kitangili Moshi Kanji akihidi kutoa gunia moja la mahindi kusaidia mpango huo.
Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga Nyanjulwa Kiyenze, amewasihi wazazi kwa shule zote za manispaa hiyo, waguswe na suala la ulaji wa chakula shuleni, na kuchangia ili wanafunzi wafanye vizuri kitaaluma.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Leah Mzanva, amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 452, na waliokuwa wakipata chakula ni madarasa ya mtihani tu la nne na saba, na kwamba wanafunzi wote wakipata chakula ufanisi wa masomo utaongezeka, sababu mwanafunzi kusoma akiwa na njaa hawezi kuelewa.
Nao baadhi ya wazazi akiwamo Winifrida Clement, wamesema wameguswa na suala la chakula shuleni na kuahidi kujitahidi kuchangia, ili watoto wao wasisome wakiwa na njaa, sababu wamejionea kwa vitendo ulaji wa chakula shuleni ulivyonafaida.
Baadhi ya wanafunzi akiwamo Yohana Paul darasa la tano, amesema wamefarijika kuzinduliwa kwa zoezi hilo la ulaji wa chakula shuleni kwao, na kwamba hawatasoma tena wakiwa na njaa, na watazingatia masomo hasa muda wa mchana ambapo hushikwa na njaa kali.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki SDO Gerald Ng'ong'a akizungumza.
Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Iwelyangula Leah Mzanva akizungumza.
Afisa Maendedeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga Nyanjula Kiyenze akizungumza.
Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki SDO Gerald Ng'ong'a akikabidhi chakula shule ya Msingi Iwelyangula.
Mkurungezi wa Shirika la Rafiki SDO Gerald Ng'ong'a akizundua zoezi la ulaji wa chakula shule ya msingi Iwelyangula.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464