` TFS YAPANDA MITI 350 SHINYANGA GIRLS KUADHIMISHA SIKU YA MISITU DUNIANI

WANDAMAN HOTEL

TFS YAPANDA MITI 350 SHINYANGA GIRLS KUADHIMISHA SIKU YA MISITU DUNIANI

 



Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Wakala wa huduma za misitu Tanzania TFS Kanda ya Magharibi, ambayo inaunganisha mikoa ya Katavi, Tabora, Kigoma na Shinyanga, wamepanda miti 350 katika shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga Girls kwa ajili ya kuhifadhi mazingira.

Upandaji huo wa miti umefanyika leo Machi 20, 2026, kuelekea maadhimisho ya siku ya misitu duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 21.

Afisa Misitu Mwandamizi na Mkuu wa Operesheni Kanda ya Magharibi (TFS) Shadrack Msilu, amesema katika maadhimisho hayo kikanda mkoani Shinyanga, wameamua kupanda miti katika shule hiyo, ili kuhamasisha jamii kupanda miti kwa vitendo katika kuhifadhi mazingira na kuacha kukata miti hovyo.
“Kila mwaka hekta za misitu 406,900 hupotea kutokana na ukataji miti holela na ndiyo maana tunatoa elimu kwa wananchi watunze mazingira kwa kupanda miti kwa wingi na kuacha kuikata, ili tukabiliane pia na mabadiliko ya tabia nchi,” amesema Msilu.

Naye Mwenyekiti wa Club ya Mazingira shuleni hapo Kabula Bundala, akisoma taarifa ya shule hiyo, amesema ilianzishwa mwaka 2023, ambapo ilikuwa na mti mmoja tu wa asili, lakini shule hiyo walishirikiana na TFS wilaya ya Shinyanga kupanda miti na sasa wanajumla ya miti 12,053.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga Said Kitinga, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya, amewataka wananchi kutunza mazingira kwa kupanda miti kwa wingi, pamoja na kutumia nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji wa miti hovyo.

Amesema kuwa matumizi ya nishati mbadala ni muhimu katika kulinda misitu, na kuhakikisha mazingira yanabaki salama kwa vizazi vijavyo.

MAELEZO KATIKA PICHA👇👇
Katibu Tawala wa wilaya ya Shinyanga Said Kitinga akizungumza.
Afisa Misitu Mwandamizi na Mkuu wa Operesheni Kanda ya Magharibi (TFS) Shadrack Msilu akizungumza.
Mwenyekiti wa Club ya Mazingira shuleni ya Sekondari Shinyanga Girls Kabula Bundala, akisoma taarifa ya shule.
Katibu Tawala wa wilaya ya Shinyanga Said Kitinga akipanda mti.
Afisa Misitu Mwandamizi na Mkuu wa Operesheni Kanda ya Magharibi (TFS) Shadrack Msilu akipanda mti.
Mkuu wa shule ya Sekondari ya Shinyanga Girls Nurah Kamuntu akipanda mti.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464