Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka akizungumza na vijana mkoani Shinyanga wakati akizundua Jukwaa la Vijana.
Na mwandishi wetu.
Waziri wa Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Arthur Nanauka, leo amezindua rasmi Jukwaa la Vijana Mkoa wa Shinyanga, akisisitiza kuwa vijana ni rasilimali ya kwanza ya maendeleo na mhimili muhimu wa uchumi wa Taifa.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika mkoani Shinyanga leo Februari 21,2026, Waziri Nanauka amesema vijana ni takribani theluthi moja ya watanzania, hivyo hawawezi kuachwa nyuma katika mchakato wa maendeleo.
“Hatuwezi kubadili nchi bila kuwekeza kwa vijana. Vijana wakipewa nafasi na mitaji, wanaweza kuendesha uchumi wa Taifa,” alisisitiza Waziri Nanauka.
Fursa za Uchumi na Sekta za Kimkakati
Katika hotuba yake, Waziri Nanauka alitaja sekta za kimkakati zinazolengwa kuwawezesha vijana, ikiwemo:madini,kilimo,mifungo,biashara,viwanda na mawasiliano akieleza kuwa kuna hatua za kuhakikisha vijana wanashiriki na kupatiwa mitaji.
Alieleza kuwa Mkoa wa Shinyanga una nafasi ya kipekee kijiografia kama lango la Kanda ya Ziwa na hata masoko ya kimataifa. Akitolea mfano, wazo la kutenga eneo maalum la viwanda katika eneo la Buzwagi (industrial shed), akisema hatua hiyo itafungua fursa zaidi za ajira na uzalishaji kwa vijana.
Aidha, aliwahimiza vijana kuanzisha ‘SHY Hub’ kama kitovu cha ubunifu na ujasiriamali kitakachowawezesha kupanua masoko yao kwa kutumia mifumo ya kidigitali.
“Serikali imeshatoa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kiuchumi. Ningependa kuona vijana wa Shinyanga wanajitokeza na kuchangamkia fursa hii ya mitaji. Fedha hizo zimesambazwa katika sekta mbalimbali, zikiwemo Wizara za Mifugo na Uvuvi; Kilimo; Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; Viwanda na Biashara; pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu.”amesema nanauka.
Ajira na Mafunzo
Akizungumzia ajira serikalini, Waziri alisema kuwa tayari kada ya elimu imeajiri walimu 7,000 huku sekta ya afya ikiajiri watumishi 5,000, ambao usajili na kuripoti kazini umekamilika.
Aidha, kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), serikali imeendelea kufungua milango ya ajira ndani na nje ya nchi. Alibainisha kuwa mikataba saba ya awali imesainiwa kwa ajira za nje, ambapo vijana 300 wamekwenda kwenda Dubai katika awamu ya kwanza. Fursa hizo zinahusisha taaluma za ufundi majengo, magari na kada nyingine za stadi.
Katika kuimarisha ujuzi, Waziri alitangaza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 3 zimetengwa kwa mafunzo ya ufundi stadi, ambapo vijana watapatiwa zana (tools) mara baada ya kuhitimu ili kuwawezesha kuanza kazi mara moja.
Urasimishaji biashara na Mikopo
Katika kipindi cha siku 100 za utawala wa serikali ya inayongozwa na Mhe,Dkt Samia, Waziri alisema ahadi 14 zimeanza kutekelezwa, ikiwemo kurahisisha masharti ya urasimishaji wa shughuli ndogo ndogo za kiuchumi kama za mama na baba lishe, kufuatia maelekezo ya Waziri wa Mkuu, Mhe.Mwigulu Nchemba, ya kulegeza masharti kwa makundi hayo katika taratibu za mikopo.
Maadili na Uongozi
Waziri Nanauka alisisitiza kuwa sera mpya inalenga kuwajengea vijana maadili, uwajibikaji na uzalendo, akibainisha kuwa taifa lina rasilimali 10 za maendeleo, lakini vijana ndiyo rasilimali namba moja.
"Maono ya Mhe.Rais Samia ni kuwa kila kijana ana uwezo wa kuwa kiongozi wa aina yoyote bila kujali historia au mazingira aliyotoka.amesema Nanauka.
Uzinduzi wa Jukwaa hilo unatarajiwa kuwa chachu ya kuibua miradi ya maendeleo mkoani Shinyanga, sambamba na kuimarisha ushiriki wa vijana katika uchumi wa kidigitali, viwanda, nishati na sekta nyingine za uzalishaji.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza kwenye uzinduzi wa Jukwaa la Vijana mkoani humo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni akizungumza.