Upandaji wa miti ya asili ukiendelea kando kando ya mto Tighite katika kijiji cha Matongo
***
Katika mwendelezo wa utelekezaji wa mkakati endelevu wa kampuni ya Barrick, Mgodi wake wa North Mara uliopo wilayani Tarime mkoani Mara umefanikisha upandaji wa miti zaidi ya 40,000 kando ya mto Tighite kwa ushirikiano na shirika lisilo la kiserikali la Jamii wa Watumiaji wa Maji Tigithe Chini (JWMTC) kwa ajili ya kuhifadhi mazingira na kurejesha na uoto wa asili.
Mto Tighite ni moja ya vyanzo vikuu vya maji vya Mto Mara ambao unatiririsha maji yake katika Ziwa Victoria upande wa Tanzania na maelfu ya wakazi wa vijiji vilivyopo jirani na mgodi wa Barrick North Mara wanategemea mto huo kupata maji ya matumizi ya nyumbani, kunywesha mifugo na shughuli za kilimo.
Akiongea kuhusu programu hiyo ambayo inaendelea kupata mafanikio, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Tigithe Chini (JWMTC), Mwita Seri, ameeleza kuwa kutokana na uwezeshaji na ushirikiano wanaoupata kutoka mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara hadi kufikia sasa wamefanikiwa kupanda miche ya miti 42,700.
“Tangu progamu hii ya kupanda miti kando ya mto Tighite izinduliwe mwaka jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani tumekuwa tukipata ushirikiano mkubwa kutoka Mgodi wa North Mara na lengo lililokusudiwa la kutunza mazingira katika eneo hili linaendelea kupata mafanikio na eneo hili la mto limebadilika kwa kiasi kikubwa sasa”, amesema Mwita Seri.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko amesema wakati wa uzinduzi wa progamu hiyo kuwa kuwa Dhamira ya mgodi ni kupanda miti ya asili 50,000 katika kingo za mto Tighite ili kuzuia mmomonyoko wa udongo kwa kushikilia udongo kwa mizizi yake ikiwemo na miti ya mbao itakayopandwa mita 60 za mto huo." Programu kama hizi ziliwahi kufanyika mto Mara . Dhumuni letu ndani ya mwaka mmoja tuwe tumekamilisha Programu hii" ,amesisitiza.
Wafanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara wakishirikiana na wananchi kupanda miti ya asili kando kando ya mto Tighite wakati wa uzinduzi wa programu hiyo mwaka 2025.
Kwa mujibu wa Seri, uharibifu mkubwa wa uoto wa asili wa mto Tighite ndio uliisukuma taasisi ya Jumuiya ya Watumia Maji Tigithe Chini (JWMTC), kubuni wazo la kuwa na mpango endelevu wa kuhifandi mazingira ya chanzo hicho cha maji.
Amesema mgodi wa Barrick North Mara unagharimia ununuzi wa miche ya miti, uchimbaji mashimo na ulinzi wa miti iliyopandwa, miongoni mwa mambo mengine katika mradi huu.“Lengo kubwa ni kulinda mto Tighite kwa kurudisha uoto wa asili, na hata miti tunayopanda ni ya asili na rafiki kwa mazingira,” amesisitiza Mwenyekiti huyo wa JWMTC.
Seri amebainisha kuwa Jumuiya ya Watumia Maji Tighite Chini ambayo iko chini ya Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, inasimamia kata nne zenye vijiji 12 jirani na mgodi wa Barrick North Mara. Alitaja vijiji hivyo na kata zake zikiwa kwenye mabano kuwa ni Matongo, Nyabichune, Nyangoto na Mjini Kati (Matongo), Nyamwaga na Komarera (Nyamwaga).
Vijiji vingine ni Nyakunguru, Nyarwana, Wegita na Keisaka (Kibasuka), Kewanja na Kerende (Kemambo).
Sehemu ya miche ya miti ya asili iliyooteshwa kwenye kitalu cha Jumuiya ya watumia maji Tighite Chini kwa ajili ya kupandwa kando kando ya mto Tighite
Mbali na kuwezesha utekelezaji wa mradi huu wa mazingira na kulinda chanzo cha maji cha mto Tighete Mgodi wa Barrick North Mara kupitia fedha za CSR umefanikisha mradi wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 2.665 kwa ajili ya upanuzi wa chanzo cha maji cha Nyamongo, wilayani Tarime vijijini kilichopo ndani ya eneo la Mgodi ambacho awali kilisanifiwa kuhudumia wananchi 27,742 wa vijiji vya Nyangoto, Matongo, Mjini Kati na Nyabichune na unasimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na uko katika hatua za mwisho kukamilika.
Kutokana na ongezeko la mahitaji ya maji katika vijiji vingine saba vinavyozunguka mgodi. Chanzo hiki kimesanifiwa upya kwa lengo la kuhudumia wananchi 125,566 katika vijiji vingine sita vya Genkuru, Nyamwaga, nyakunguru, Kerende, Msege na Komarera.
Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Kampuni ya Barrick kupitia utekelezaji wake wa mkakati endelevu inaendelea kufanikisha miradi mbalimbali ya kijamii katika maeneo yanayozunguka migodi yake hususani katika kuboresha sekta ya elimu, upatikanaji wa maji salama, afya, mazingira na kuongea wigo kwa ajira.


