Kaimu Afisa Uhamiaji na Mkaguzi wa Uhamiaji wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Robert Mahenge akitoa elimu kuhusu Uhamiaji, Uraia, Pasipoti na Hati za Safari sambamba na Kampeni ya “Mjue Jirani Yako” kwa walimu na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kilichopo Kata ya Igaga Februalri 11,2025
Na Sumai Salum – Kishapu
Katika kuimarisha usalama wa Nchi na kuwajengea vijana uelewa mpana wa masuala ya kisheria, Idara ya Uhamiaji Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Februari 11, 2026 imetoa elimu ya kina kuhusu Uhamiaji, Uraia, Pasipoti na Hati za Safari sambamba na Kampeni ya “Mjue Jirani Yako” kwa walimu na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Kishapu kilichopo Kata ya Igaga.
Elimu hiyo imetolewa na timu iliyoongozwa na Kaimu Afisa wa Uhamiaji Wilayani humo Robert Mahenge, ambapo walimu pamoja na zaidi ya wanafunzi 100 wanaosoma fani za Umeme, Ushonaji na Ufundi Magari wamepata fursa ya kufahamu wajibu wao katika kulinda mipaka na maslahi ya nchi.
Akizungumza wakati wa semina hiyo, Mahenge amesema Ofisi ya Uhamiaji si chombo cha kudhibiti tu, bali ni taasisi ya kutoa huduma na kushirikiana na wananchi kuhakikisha taratibu zote za kisheria zinafuatwa kwa manufaa ya taifa.
Amesisitiza kuwa uzalendo ni nguzo muhimu katika kulinda usalama wa nchi, akiwataka walimu na wanafunzi kuwa mabalozi wazuri kwa jamii kwa kuwa macho na kutoa taarifa sahihi pale wanapobaini uwepo wa wageni wasiokuwa na vibali halali.
“Usalama wa nchi unaanzia kwa mwananchi mmoja mmoja. Tunaposhirikiana na mamlaka husika, tunalinda ajira zetu, rasilimali zetu na mustakabali wa taifa letu,” amesisitiza.
Amefafanua kuwa wapo wageni wasiokuwa raia wanaoingia nchini kwa njia zisizo halali kwa lengo la kuoa au kuolewa, kuajiriwa au kushiriki shughuli za kiuchumi kama kilimo na ufugaji bila kufuata sheria. Hivyo, amewataka wananchi wote wanaoingia mahusiano au kuajiri raia wa kigeni kuhakikisha wanapata mwongozo kutoka Ofisi za Uhamiaji ili kuepuka kuvunja sheria bila kujua.
Kupitia Kampeni ya “Mjue Jirani Yako”, washiriki wamekumbushwa umuhimu wa kufahamu watu wanaoishi nao katika maeneo yao ili kusaidia kudhibiti wahamiaji haramu na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na usalama.
Sambamba na hilo, wanafunzi walipatiwa elimu kuhusu umuhimu wa kuwa na pasipoti na hati za safari mapema kama sehemu ya maandalizi ya kutumia fursa za ajira, masomo au biashara nje ya nchi. Ikielezwa kuwa gharama ya pasipoti ni Shilingi 150,000 na hati ya safari ya dharura ni Shilingi 20,000, huku wakihimizwa kutosubiri hadi siku ya safari ndipo waanze mchakato wa maombi.
Kwa niaba ya wanafunzi, Gloria Justus Dominick, mwanafunzi wa fani ya Umeme, amesema elimu hiyo imewafungua macho na kuwajengea uelewa mpana kuhusu wajibu wao kama vijana katika kulinda taifa.
“Mbali na taaluma tunazosoma, tumepata maarifa yatakayotusaidia kuwa raia wema na kuwasaidia wengine kuelewa masuala ya uhamiaji na usalama,” amesema.
Mkufunzi Domician Mjuni, kwa niaba ya uongozi wa chuo hicho, ameishukuru Idara ya Uhamiaji kwa kuwafikia chuoni hapo na kueleza kuwa elimu hiyo imeongeza uelewa kwa walimu na wanafunzi kuhusu sheria na taratibu za uhamiaji.
Ameahidi kuwa chuo kitaendelea kushirikiana na Ofisi ya Uhamiaji kwa kutoa taarifa za wanafunzi raia wa kigeni na kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa kwa mujibu wa sheria, hatua itakayosaidia kuimarisha udhibiti wa wahamiaji haramu katika Wilaya ya Kishapu.





.jpg)
.jpg)

