` BANDIKA BANDUA YA MAPINGAMIZI MKAKATI DHAIFU WA LISU WA KUTAKA UMAARUFU

BANDIKA BANDUA YA MAPINGAMIZI MKAKATI DHAIFU WA LISU WA KUTAKA UMAARUFU

KATIKA kile kinachoonekana kama mchezo wa "paka na panya" ndani ya kuta za mahakama, mwenendo wa kesi Na. 19605/2025 inayomkabili mwanasiasa Tundu Lissu umezua mjadala mzito kuhusu tija ya kisheria na matumizi ya muda wa chombo hicho huru. 

Wakati Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Ndugu John Heche, akijitokeza hadharani kuhoji kuchelewa kwa kesi hiyo, ukweli mchungu unaoibuka ni kuwa "mwenye kesi" anaonekana kuwa ndiye kikwazo kikuu cha utatuzi wa haraka wa shauri lake.

Uchambuzi wa mwenendo wa kesi hiyo unaonyesha kuwa bandika bandua ya mapingamizi yasiyo na afya yamegeuka kuwa silaha ya kuchelewesha utekelezaji wa haki. 

Mapingamizi zaidi ya saba yaliyowekwa na upande wa mshitakiwa, kuanzia kupinga uhalali wa hati ya mashitaka hadi kupinga kanuni za ulinzi wa mashahidi, yameiteka mahakama na kuifanya ishindwe kuingia kwenye shauri la msingi. Wataalamu wa sheria wanatazama utitiri huu wa mapingamizi kama nia ovu ya kuipotezea mahakama muda kimbinu kwa maslahi binafsi.

Inadaiwa kuwa Tundu Lissu ameigeuza kesi hii kuwa "mradi wa kiuchumi" kwa ajili yake, familia yake, na chama chake. Mkakati huu unatajwa kulenga mambo mawili makuu: Kwanza, kuendelea kupata fedha kutoka kwa wafadhili wa nje kwa kisingizio cha mateso ya kisheria, na pili, kuendeleza kelele za kisiasa kuwa anaonewa. 

Hali hii ya kupika mapingamizi ili kesi isiishe haraka, inazua maswali juu ya utu na uadilifu katika kutafuta haki, huku ikididimiza heshima ya chombo hicho ambacho kinapaswa kufanya kazi kwa uhuru na uwazi.

Ni wakati sasa kwa wanasiasa kama Ndugu Heche kuwa waeli na kutazama upande wa pili wa sarafu. Mapingamizi mara kwa mara yanahatarisha utekelezaji wa haki kwa wahusika wote na yanadumaza mfumo wa sheria nchini.

 Kama kweli nia ni kupata haki, mshitakiwa anapaswa kuacha kutumia muda mwingi kuelezea masuala yasiyo ya kisheria, kama maisha ya mahabusu, na badala yake kuruhusu hoja za msingi kusikilizwa. Bila tathmini ya kina, kesi hii itaendelea kuwa uwanja wa kuvuna fedha badala ya kutafuta ukweli, jambo ambalo halina afya kwa ustawi wa taifa letu.

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464