Wakati 'wahuni' wachache wakihaha usiku na mchana kutafuta kila mbinu ya kuchafua taswira ya Tanzania na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita, jumuiya ya kimataifa imeendelea kutoa jibu la mapigo linaloonesha kuwa Mama anatosha na kazi inaonekana.
Shirika la Kimataifa la Tathmini za Kiuchumi la Moody’s Ratings, katika ripoti yake ya Februari 20, 2026, limeipandisha chati Tanzania kwa kuipa alama ya B1 (Stable). Alama hii si namba tu, bali ni tusi la nguoni kwa wale wote waliokuwa wanatabiri anguko la uchumi wetu baada ya vuguvugu la kisiasa la Oktoba mwaka jana. Moody’s wamesema wazi: Tanzania ni imara, uchumi unapaa, na mtazamo ni thabiti!
Licha ya kelele za hapa na pale, ripoti hiyo inabainisha kuwa uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia sita (6%) mwaka huu. Hii ni matokeo ya kazi ya kishujaa ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kufungua nchi kupitia sekta za utalii, madini, na viwanda.
Wakati wahujumu wakitamani kuona Serikali inashindwa, maboresho ya usimamizi wa kodi na uwekezaji mkubwa kwenye mifumo ya kidijitali umesaidia mapato yasiyo ya ruzuku kupanda kutoka asilimia 13.7 (2020/21) hadi kufikia asilimia 15.9 na sasa inakimbilia asilimia 17! Huu ni ushindi wa kishindo kwa sera za uchumi za Awamu ya Sita.
Kuhusu deni la Serikali ambalo limekuwa likitumiwa na wapinzani kama 'fimbo' ya kupigia, Moody’s wamewatolea uvivu. Ripoti imethibitisha kuwa deni la Tanzania ni la wastani na linabaki kuwa imara kwa asilimia 50 ya Pato la Taifa (GDP). Sababu? Serikali haikopi kwa ajili ya anasa, bali kwa ajili ya miundombinu ya kimkakati (SGR, Bwawa la Nyerere) na huduma za kijamii zinazogusa maisha ya mnyonge.
Mtendaji Mkuu wa Benki ya Stanbic Tanzania, Manzi Rwegasira, amethibitisha kuwa tathmini hii ya Moody’s ni 'cheti cha ushindi' kinachoonesha kuwa nchi inaaminika kimataifa. Amesema imani ya wawekezaji kwa Tanzania sasa iko juu kuliko wakati mwingine wowote, jambo ambalo litaendelea kupunguza gharama za mikopo.
Hata wataalamu wa madeni waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina, wamekiri kuwa kuna wadau waliojificha walikuwa 'wanasubiri kwa hamu' kuona Tanzania inapata alama hasi baada ya uchuguzi wa Oktoba 29. Lakini, uthabiti wa Mama Samia na busara za Serikali yake zimezima ndoto hizo za mchana, na badala yake wawekezaji wanazidi kumiminika nchini.
Ukweli unabaki kuwa: Dunia inatuona, na inatuona vyema! Maboresho ya miundombinu ya nishati na usafiri yanayofanywa na Serikali yanazidi kufifisha shinikizo la kijamii na kuleta ustawi. Hii ni salamu kwa wale wote wanaotaka kurudisha nyuma Mwelekeo wa uchumi: Tanzania ya sasa si ya kuchezea, inasonga mbele kwa mshikamano wa dhati na uongozi uliotukuka.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464