` TANZANIA NI MOJA, TUSIITIE KIBERITI KWA UBINAFSI WETU: AMANI NDIO MTAJI WA PEKEE WA MAENDELEO

TANZANIA NI MOJA, TUSIITIE KIBERITI KWA UBINAFSI WETU: AMANI NDIO MTAJI WA PEKEE WA MAENDELEO



Katika nyakati ambapo dunia inashuhudia machafuko na mitafaruku, sauti za uzalendo zimeendelea kurindima nchini Tanzania, zikiwakumbusha raia kuwa amani si zawadi, bali ni ngao na urithi ambao lazima ulindwe kwa gharama yoyote.
Huu ni ujumbe uliotawala ziara ya Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, mkoani Tabora, ukirejelewa pia na viongozi wa kidini na kijamii nchini.

Akizungumza na wakazi wa Puge wilayani Nzega Februari 16, 2026, Kihongosi amesisitiza kuwa Watanzania ndio "walinzi namba moja" wa amani ya nchi yao.

"Amani ndiyo msingi wa kila kitu; uwekezaji, elimu ya VETA tunayoihubiri, na matibabu ya kibingwa Muhimbili yote yanategemea utulivu. Tusikubali mtu yeyote atugawanye kwa maslahi yake binafsi," alisema Kihongosi huku akipokelewa kwa shangwe na wananchi.

Hoja hiyo imeungwa mkono na Mwenyekiti wa JMAT Wilaya ya Mkuranga, Shukuru Ngweshani, aliyebainisha kuwa nchi yetu haina "spea".

"Tukiipiga kiberiti nchi yetu, hatuna kwingine kwa kwenda. Lazima tuaminiane na tufanye kazi pamoja bila ubaguzi," alisisitiza. Kauli hiyo inaakisi maoni ya wazalendo wengi wanaokerwa na wale wanaotumia mitandao ya kijamii kuchochea hasira na migawanyiko.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ATF, Rosemary Bujashi, amewakumbusha Watanzania kuwa amani ndiyo inatukinga na wasioitakia mema nchi yetu. Huku akisisitiza umuhimu wa akina mama katika kulea familia kwenye misingi ya upendo, amemtaja Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kama mfano wa kiongozi anayesimamia amani ili kila Mtanzania aweze "kula ugali wake kwa raha" na kujiendeleza kiuchumi.

Diwani wa Mkuranga, Hamza Mahanaka, ametoa onyo kwa vijana kutoingia kwenye makundi yanayoweza kuyumbisha nchi kiuchumi. "Utulivu unamfanya mwekezaji aje, unamfanya mkulima aende shambani bila hofu," alisema.

Ujumbe huu ni jibu tosha kwa wale wanaodhani kuwa kupaza sauti za chuki ni sifa. Ukweli unabaki kuwa, Tanzania ni nyumba yetu sote. Tutaishi hapa, tutafanya biashara hapa, na tutazikwa hapa. Kulinda amani si chaguo, ni wajibu wa kila mzalendo anayeitakia mema nchi ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464