
Uimara wa mhimili wa Mahakama unategemea utayari wa viongozi wake kutenda kazi kwa uaminifu na kuzingatia viapo vyao bila kutetereka wala kusubiri kuelekezwa jambo ambalo liko ndani ya uwezo wao, anasema Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. George Masaju.
Prof. Masaju, amesisitiza kuwa tangu aingie madarakani, kipaumbele chake kimekuwa ni kuona watumishi wanajituma si kwa sababu ya shinikizo la mtu, bali kwa kutambua kuwa ni wajibu wao wa kisheria na kikatiba kutoa haki kwa wakati na kwa haki.
Jaji Mkuu Masaju ametoa msimamo huo jijini Dodoma mnamo Februari 25, 2026, wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Mwaka cha Majaji Wafawidhi, ambapo amebainisha kuwa utoaji haki nchini hauwezi kuendeshwa kwa utaratibu wa kusubiri maelekezo kutoka mamlaka za juu.
Amesema kuwa kila kiongozi mwenye dhamana anapaswa kuongozwa na weledi na uwajibikaji wa hiari, kwani viongozi hao ni binadamu wenye akili na uelewa wa kutosha wa wajibu wao kikatiba.
Aidha, Jaji Mkuu amefafanua kuwa kusubiri maelekezo ya kila siku ili kutimiza majukumu ni kudhoofisha ufanisi na kunaweza kuharibu mahusiano ya kikazi na kushusha hadhi ya taasisi hiyo ambayo ni kimbilio la mwisho la wananchi.
Amesisitiza kuwa mahakama lazima iwe mfano wa kuigwa kwa taasisi nyingine nchini, na ameonya dhidi ya utamaduni wa viongozi kuzungumza kwenye vikao na kisha kusubiri vikao vingine bila kutekeleza yale yaliyoafikiwa kwa wakati.
Msimamo huu unalenga kuimarisha uhuru wa mahakama na kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri kwa maslahi ya Taifa.
Jaji Mkuu amehitimisha kwa kusema kuwa kila Jaji na kiongozi wa mahakama anapaswa kutumia mamlaka yake kulingana na sheria ili kuleta matokeo chanya kwa jamii, jambo ambalo litaongeza imani ya wananchi kwa mhimili huo muhimu wa utoaji haki
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464