` HALMASHAURI YA WILAYA YA ARUSHA YAENDELEA KUBORESHA MAKAZI YA WALIMU

HALMASHAURI YA WILAYA YA ARUSHA YAENDELEA KUBORESHA MAKAZI YA WALIMU



Na Bora Mustafa,Arusha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (DC), Bw. Sulemani Msumi, amesema halmashauri hiyo inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa watumishi wake, ikiwemo walimu, hususan katika kata za pembezoni kwa kuwajengea nyumba za kuishi.

Amesema  hayo Februari 26,2026 kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali kupitia Halmashauri hiyo imefanikiwa kujenga nyumba za walimu katika shule nne zilizopo katika kata tofauti. 

Hatua hiyo inalenga kupunguza changamoto ya walimu kutembea umbali mrefu kwenda kutoa huduma kwa wanafunzi, pamoja na kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi katika sekta ya elimu.

Aidha,amesema  katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu, halmashauri imetenga shilingi milioni 40 kwa ajili ya Shule ya Sekondari Likamba kwa ukamilishaji wa nyumba tatu za walimu.

  Pia Amesisitiza kuwa mpango huo ni endelevu na utanufaisha si walimu pekee bali pia watumishi wengine wa halmashauri hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, Baraka Mesiaki, amesema katika kikao cha baraza la kawaida (Full Council), madiwani walijadili masuala mbalimbali yanayogusa maendeleo ya wananchi katika kata zote 27.

Ameeleza kuwa miongoni mwa ajenda zilizopewa kipaumbele ni maboresho ya utoaji wa mikopo kwa wanawake, vijana na makundi maalum. Pia, walijadili namna bora ya kurejesha mikopo iliyochukuliwa na vikundi, hasa pale ambapo baadhi ya wanachama walishindwa kurejesha kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo vifo.

Hata hivyo, madiwani wamekubaliana kuunda kamati rasmi itakayowahusisha pia mabalozi wa mitaa, ili kuhakikisha vikundi vinavyokopa vinakuwa na taarifa sahihi na kumbukumbu kamili kupitia kwa balozi husika. Kwa kuwa mabalozi ni viongozi wanaowafahamu wananchi wao kwa karibu, hatua hiyo inatarajiwa kurahisisha ufuatiliaji na marejesho ya mikopo.

Katika hatua nyingine, halmashauri hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 600 katika kipindi cha nusu mwaka kuanzia Oktoba hadi Desemba 2025, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuinua uchumi wa wananchi na kuchochea maendeleo katika jamii.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464