` CRDB FOUNDATION SASA TAYARI KUENDESHA MFUKO WA MAENDELEO YA VIJANA

CRDB FOUNDATION SASA TAYARI KUENDESHA MFUKO WA MAENDELEO YA VIJANA

Hatua ya kihistoria ya kusainiwa kwa hati ya makubaliano kati ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana na Benki ya CRDB kupitia CRDB Bank Foundation kwa ajili ya uendeshaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ina maana kubwa sana kwa mustakabali wa ajira, amani, na utulivu hapa nchini.
Makubalano hayo yanafungua milango mipya ya ajira kwa maelfu ya vijana ambao sasa watapata mitaji ya kuanzisha na kukuza miradi ya ujasiriamali, ubunifu, na maendeleo ya kiuchumi.

Upatikanaji wa mikopo nafuu kupitia ushirikiano huu rasmi unakwenda kuondoa kisingizio cha ukosefu wa mtaji na kutoa fursa kwa vijana kuwa wazalishaji mali badala ya kuwa watafuta kazi pekee, jambo ambalo linaongeza tija na ustawi wa kijamii na kitaaluma nchini.

Kiuweledi, uwezeshaji huu mkubwa wa kiuchumi ni mhimili mkuu wa kudumisha amani na utulivu kwani vijana wakiwa na shughuli za kuwaingizia kipato na miradi ya kujiendeleza, wanakuwa na matumaini ya maisha na kuepuka kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa taifa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka amesisitiza kuwa mfuko huu ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwaandaa vijana kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa, jambo linalojenga msingi wa kizazi chenye tija na mshikamano.

Mfuko huo umeanzishwa kwa hundi ya Sh bilioni 200 iliyokabidhiwa wizara hiyo na Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan umelenga kuwezesha vijana, hali itakayochochea utulivu kwa kupunguza manung'uniko ya kiuchumi na kuimarisha imani ya wananchi kwa serikali yao katika safari ya kuelekea uchumi jumuishi.




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464