` MADIWANI MANISPAA YA SHINYANGA WAPITISHA BAJETI YA BILIONI 42.2 MWAKA WA FEDHA 2026/2027

MADIWANI MANISPAA YA SHINYANGA WAPITISHA BAJETI YA BILIONI 42.2 MWAKA WA FEDHA 2026/2027

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wamepitisha bajeti ya sh. bilioni 42.2, kwa mwaka wa fedha 2026/2027, kwa ajili ya kuendesha shughuli za utoaji huduma, utawala na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Bajeti hiyo imepitishwa leo Februari 19, 2026 katika kikao maalumu cha baraza la madiwani, kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.

Awali Mchumi wa Manispaa ya Shinyanga Mensari Mrema, akisoma makisio ya bajeti hiyo, amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027 wanatarajia kukusanya na kutumia sh.bilioni 42.2.
“Makisio ya matumizi ya fedha, kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Jumla ya sh. bilioni 42.2 zinatarajiwa kutumika katika shughuli mbalimbali za utoaji huduma, utawala ,na utekelezaji wa maendeleo kwa wananchi,”amesema Mrema.

Baada ya mjadala wa kina uliohusisha madiwani kuchangia na kutoa mapendekezo mbalimbali, Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo, alihoji iwapo wajumbe wameridhia kuipitisha bajeti hiyo, ambapo kwa kauli moja waliipitisha.
Kitumbo akizungumza mara baada ya madiwani kupitisha bajeti hiyo, amewataka wataalamu kuhakikisha mapendekezo yote yaliyotolewa yanatekelezwa kwa vitendo ili kufanikisha malengo ya maendeleo ya manispaa hiyo.

“Bajeti hii ni mkataba baina ya madiwani na wananchi ,yote yale ambayo tumejadili na kukubaliana yazingatiwe ,ili tulete tabasamu kwa wananchi wetu kwa kutatua kero mbalimbali,” amesema Kitumbo.
Nao baadhi ya Madiwani akiwamo Ruben Kitinya wakijadili bajeti hiyo, ameshauri kuendelea kuibuliwa vyanzo vipya vya mapato ya ndani, huku akipongeza kwenye bajeti hiyo kuwepo na ununuzi wa mtambo wa halmashauri wa utengenezaji barabara, hali ambayo itasaidia ufunguaji wa barabara nyingi za mitaa.

TAZAMA PICHA👇👇
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo akizungumza.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo akiongoza kikao cha baraza cha bajeti.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Jackson Mwakisu akizungumza .
Mchumi wa Manispaa ya Shinyanga Mensari Mrema, akiwasilisha makisio ya bajeti ya 2026/ 2027 kwenye kikao cha baraza la madiwani.
Baraza la bajeti likiendelea.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464