` SHUWASA KINARA TUZO YA UFANISI WA UENDESHAJI MAMLAKA ZA MAJI NCHINI

SHUWASA KINARA TUZO YA UFANISI WA UENDESHAJI MAMLAKA ZA MAJI NCHINI

SHUWASA yapokea Tuzo ya Ufanisi wa Uendeshaji

****
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imeibuka mshindi wa Tuzo ya Ufanisi wa Uendeshaji (Operational Efficiency ExcellenceAward) ikiwa ni miongoni mwa Mamlaka za Maji nchini zenye wateja zaidi ya 20,000 (Elfu Ishirini).

 Tuzo hizo zimetolewa na Wizara ya Maji katika Mkutano wa Bodi za Wakurugenzi wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Nchini - Jijini Arusha.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amekabidhi tuzo kwa washindi na kupongeza hatua kubwa ya maendeleo katika Sekta ya Maji.

Hafla ya utoaji wa tuzo hizo imefanyika huku ikishuhudiwa na wajumbe zaidi ya 1000 wanaoshiriki kwenye Mkutano na Mafunzo kwa Wajumbe wa Bodi na Menejimenti za Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira.

Waziri wa Maji amesema watendaji bado wanajukumu la kuhakikisha wanavuka vikwazo vyote vinavyowakwamisha kufikia asilimia Mia Moja ya malengo waliyokusudia.

Amesisitiza upendo kwa kila mmoja pamoja na matumizi ya teknolojia na ubunifu katika kutatua changamoto za wananchi vizingatiwe.

Tuzo hizi zimetolewa kufuatia tathmini ya kina iliyofanywa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na EWURA ikilenga kupima Utendaji Kazi maeneo mbalimbali ikiwemo uwezo wa kutatua changamoto za wananchi kwa haraka, uwezo katika kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na matumizi sahihi ya mapato.

SHUWASA imeonesha viwango bora vya uendelevu wa huduma, uwajibikaji, uwazi na matumizi bora ya rasilimali, jambo lililochangia kutwaa tuzo hiyo ya heshima.

Aidha, Mafanikio na Mshikamano wa Wananchi wa Manispaa ya Shinyanga, Tinde, Miji midogo ya Didia na Iselamagazi umechangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa Tuzo hii.

 Tuzo hii pia inaonesha jitihada zinazofanywa na SHUWASA katika kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora ya maji safi na salama. 

Mafanikio hayo yanatajwa kuongeza hamasa kwa watumishi wa Mamlaka kwa kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma ya Maji safi na Usafi wa Mazingira.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464